Timu ya majaji wa shindano ya kutafuta vipaji nchini, Bongo Star Search (BSS) imeweka wazi mambo muhimu wanayowafanyia washiriki wa mashindano hayo nyuma ya kinachoonekana kwenye kipindi cha televisheni.

‘Jaji Mkuu’ wa BSS ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya Benchmark inayoandaa mashindano hayo, Rita Paulsen amesema kuwa timu yao huwaajiri wakufunzi wenye elimu ya hali ya juu ya muziki kwa ajili ya kuwafua washiriki kuwa wanamuziki.

Madam Rita ambaye aliongozana na majaji wengine wa shindano hilo ambao ni Salama Jabir na Master Jay kwenye The Playlist ya Times Fm, alisema kuwa hutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwalipa wakufunzi hao ambao mbali na kuwafunza washiriki jinsi ya kuimba, huwapa darasa kubwa la uandishi wa nyimbo.

“Washiriki wakienda kambini tuna-hire (tunakodi) a professional trainer (mkufunzi mweledi) ambaye anakuwa analipwa kiwango cha juu sana. Mtu yeyote ambaye amepitia BSS muulize, wamefundishwa muziki hadi kuanzia kuandika muziki,” alisema Madam Rita.

“Wanafundishwa, kuna vocal training (mafunzo ya sauti), kuna choreographer (mwalimu wa kutumbuiza/kucheza) ambaye huwafundisha jinsi ya kutumbuiza jukwaani. Kwahiyo akitoka pale, labda ashindwe tu kujiongeza,” alifunguka.

Katika hatua nyingine, Master Jay ameeleza kuwa yeye hujihusisha zaidi na namna ya upangaji wa sauti na mambo mengine akiwa kama mtayarishaji mkongwe mwenye uwezo mkubwa na elimu ya ‘sound engineering’.

BSS imerejea tena mwaka huu ikiwa ni msimu wa tisa na yataanza Septemba  jijini Mwanza, ikilenga majiji makubwa manne. Mbali na Mwanza, Mbeya, Arusha na Dar es Salaam yatazalisha washiriki. 

 

Atiwa mbaroni kutoa ofa vinywaji vyenye vilevi na kubaka wadada Dar, Mwanza, Arusha
CUF waiwekea ngumu Chadema, wasema hang’oki mtu