Jeshi la Polisi nchini Uganda, limetumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandishi wa Habari takribani 50, waliokuwa wanaandamana kuelekea makao makuu ya Polisi Jijini Kampala ili wawasilishe kero zao juu ya ukatili wa Polisi dhidi yao.

Waandishi hao kutoka chama cha waandishi wa Habari wa Uganda (UJA), walikuwa wanaenda kukutana na Mkuu wa Polisi kumuomba ufanyike uchunguzi juu ya ukatili wanaofanyiwa wanahabari wakiwa katika majukumu yao na polisi watakao kutwa na hatia wachukuliwe hatua.

Katika zoezi la kuwatawanya wanahabari hao walioandamana, Baadhi yao walikamatwa na Polisi na wakapelekwa kituo cha Polisi cha kati kilichopo Jiji humo.

Imeelezwa kuwa wiki jana Polisi waliwafanyia vitendo vya ukatili na udhalilishaji waandishi wa habari wanne waliokwenda kuripoti habari ya wanafunzi kugoma katika chuo kikuu Makerere, ambapo wanafunzi walikuwa wanapinga pngezeko la asilimia 15 ya ada.

Msemaji wa Polisi, Onyango Patrick amesema malalamiko ya Wanahabari yamepokelewa na yatafikishwa sehemu husika, na kusisitiza kuwa waandishi wa Habari na Polisi watakiwa kuheshimiana.

” Kila mmoja anahitaji kuelewa kazi za mwenzake, Kama mwandishi natakiwa kufanya nini? kama polisi natakiwa kufanya nini wakati wa maandamano?, Hivyo tunahitajiana wote hatupo sawa” amesema Onyango.

UN yatuma misaada ya dharura Somalia
Masauni alia na wananchi wanaoozea jela