Mwenyekiti wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad ametoa mtazamo wake kuhusu uamuzi wa aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiungwa mkono na vyama vya upinzani vilivyounda ‘Ukawa’, Edward Lowassa kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Maalim Seif ambaye mwaka 2015 alikuwa mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) kilichokuwa mshirika wa umoja huo, amesema yeye hawezi kumhukumu Lowassa kwa uamuzi wake ingawa anakiri amewaumiza na kuwaangusha wapinzani kwa uamuzi wake huo.

Amesema Waziri Mkuu huyo wa zamani alikuwa na sababu nyingi za kumfanya arudi CCM ikiwa ni pamoja na msukumo wa familia lakini pia kutotendewa vyema na chama hicho kikuu cha upinzani.

Amesema kuwa Lowassa ni tofauti na yeye kwakuwa yeye ameweza kuvumilia mikikimikiki na matokeo ya kuwa mpinzani.

“Yule [Lowassa] ujue alikuwa Waziri Mkuu, na malupulupu yake yote ya Uwaziri Mkuu, kwahiyo baada ya kuona lile ambalo alilitegemea kupata katika upinzani hakupata, na akaona kwamba Serikali inamsindikiza…,” alisema.

“Na ninavyosikia mimi familia yake ilimshinikiza, kwamba kuna mmoja kati ya wakwe zake alikuwa gerezani na watoto wake walikuwa wanamwambia ‘baba unaona… baba yetu sisi anapata shida kwa sababu wewe uko upinzani. Kwahiyo, ile presha ya familia ilikuwa kubwa sana. Lakini vilevile tunasikia pia kuwa na Chadema hawakumtendea vyema vilevile… kwahiyo ana sababu nyingi na mimi sitaki kumhukumu, lakini tulivunjika moyo sana [Lowassa kurudi CCM],” Maalim Seif aliiambia Global TV.

Mwanasiasa huyo alikiri kuwa ujio wa Lowassa ndani ya Ukawa ulisaidia na kuongeza nguvu kubwa ya umoja huo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ingawa hawakufanikiwa.

Machi 1, 2019, Lowassa alirejea rasmi CCM aliyoihama mwaka 2015 baada ya kuondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kupata nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

GSM wasitisha huduma Young Africans
Mwanamuziki mkongwe Afrika afariki dunia kwa Corona