Chama cha Wananchi (CUF) upande wa mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba umedai Maalim Seif Sharif Hamad anajiandaa kuhamia ACT-Wazalendo.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa CUF, Khalifa Suleiman Khalifa ambapo amedai vyama sita vya upinzani vilivyokutana Zanzibar wiki iliyopita moja ya ajenda yao ilikuwa namna gani Maalim Seif atakubaliana na ACT-Wazalendo.

Amesema miongoni mwa makubaliano hayo ni kuwa upande wa Maalim Seif uachiwe nafasi zote za uongozi upande wa Zanzibar na Zitto Kabwe ambaye ni kiongozi wa ACT- Wazalendo wachukue uongozi wa Tanzania Bara.

Aidha, amedai kuwa hata kama Maalim Seif ataondoka CUF, wataendelea kuwa imara huku akiwataka wote watakaoambatana na katibu mkuu huyo kwenda ACT- Wazalendo kutosita kwa sababu uamuzi wao utaheshimiwa.

Hata hivyo, mgogoro ndani ya CUF ulianza baada ya Lipumba kurejea katika uongozi mwaka 2016, ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu alipojiuzulu. Jambo hilo liliibua mgogoro wa uongozi baada ya ofisi ya msajili kutangaza kumtambua Lipumba kama mwenyekiti na kusababisha pande hizo mbili kukimbilia mahakamani na kufungua kesi kadhaa ambazo zinaendelea.

Imani ya ushirikina yatanda Njombe.
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 27, 2018