Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ametangaza kuhamia Chama cha ACT- Wazalendo, zikiwa zimepita saa chache tangu Mahakama Kuu ya Tanzania kuhalalisha uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba ndani ya CUF.

Maalim Seif ametangaza uamuzi huo yeye, viongozi, pamoja na wafuasi wanaomuunga mkono mapema leo Machi 18, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za wabunge wa CUF Magomeni jijini Dar es Salaam,

“Nawatangazia Watanzania wote na wanachama wote waliokuwa wanatuunga mkono mimi na wenzangu, tunajiunga na ACT- Wazalendo, tunawaomba wote wajiunge ili kuendeleza kazi kubwa tuliyokuwa tumeianza,” amesema.

Amesema kuwa mapambano ya kisiasa lazima yaendelee. “Mapambano ya kujenga demokrasia sio kazi ya lele mama, tumefanya kazi kubwa hadi hapa tulipofikia. Mimi na wenzangu, tumetafakari kwa kina juu ya uamuzi wa kesi ulivyokwenda, tumeona kutafuta jukwaa jingine la kulitumia kuwa ni ACT- Wazalendo,” amesema Maalim Seif.

Aidha, amewashukuru wale wote waliojitolea nyumba zao kwa ajili ya ofisi za CUF na kuomba waendelee kufanya hivyo wakiwa ACT- Wazalendo.

Amesema wanahamia huko pasina masharti wala vyeo na wanakwenda kama wanachama wa kawaida na ikiwa watapewa vyeo watavichukua au la.

Askari watiwa mbaroni kwa kumchapa vibao dereva, Masauni athibitisha
Mume apewa talaka kwa kujifanya kiziwi kwa miaka 62 akwepa kusikia maneno ya mkewe