Wagonga nyundo wa jijini London (West Ham United) wamemsajili mshambuliaji kutoka nchini Hispania Lucas Perez, akitokea kwa majirani zao Arsenal kwa mkataba wa miaka mitatu.

Perez mwenye umri wa miaka 29, anakuwa mchezaji wanane kusajiliwa na klabu hiyo tangu kuwasili kwa meneja mpya Manuel Pellegrini, akitanguliwa na Ryan Fredericks, Lukasz Fabianski, Issa Diop, Jack Wilshere, Aindriy Yarmolenko, Fabian Balbuena na Felipe Anderson.

“Ninafuraha ya kuwa hapa kwa ajili ya kutengeza historia ya klabu hii kubwa jijini London,” alisema mshambuliaji huyo.

“Nimefarijika sana kuwa sehemu ya kikosi cha West Ham Utd, ninaamini mipango iliopo klabuni hapa itaniwezesha kufanya vizuri kwa kushirikiana na wengine, ili kukamilisha mikakati iliyowekwa na uongozi.

“West Ham Utd ina mashabiki wanaofahamu thamani ya utu wa wachezaji wao, na hilo imekua sehemu ya sababu zilizonivuta na kukubali kujiunga na klabu hii.”

Perez alijiunga na Arsenal miaka miwili iliyopita akitokea Deportivo La Coruna kwa ada ya Pauni milioni 17, na alicheza michezo 11 huku akifunga mabao matatu (hat-trick) katika mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya FC Basel.

Msimu uliopita alishindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza na kujikuta akirejeshwa Deportivo La Coruna kwa mkopo.

Keylor Navas atangaza vita Real Madrid
Jafo ateta na viongozi kuhusu mapato ya halmashauri

Comments

comments