Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana alikamilisha zoezi la kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku akitoa ahadi yake kwa watanzania kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Oktoba.

Akiongea baada ya kuchukua fomu hizo, Lowassa alisema kuwa anaamini akiwa ndani ya Chadema na Ukawa watashinda uchaguzi mkuu ujao na kwamba hawatatumia lugha za matusi na kashfa dhidi ya wapinzani wao (CCM) bali hoja ndiyo silaha muhimu.

“Mimi ninaridhika kuwa watanzania wanataka mabadiliko na mabadiliko haya tutayapata kwa kura zetu.  Watanzania wanaotaka mabadiliko ni wengi, kwa hiyo nina uhakika tukiji-   organize vizuri tutashinda uchaguzi huu bila matatizo yoyote. Wala hatutatumia matusi, hatutatumia kejeli, tutakwenda hoja kwa hoja,” alisema Lowassa.

Akizungumzia mtazamo wa wale wanaombeza kuwa ni mtu mwenye uchu na madaraka, Lowassa amesema kuwa anachowaeleza ni kwamba yeye anatekeleza kile alichokisema Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwa watanzania wanataka mabadiliko na kwamba wasipoyapata CCM watayatafuta nje ya CCM.

Lowassa anatarajia kutambulishwa rasmi kuwa mgombea urais baada ya vikao vya Kamati Kuu ya Chadema kupitia majina ya wagombea mapema mwezi Agosti, ambapo jina lake litawasilishwa pia kwenye ngome ya Ukawa ili lipate Baraka za umoja huo.

Hata hivyo, Lowassa anaonekana kuwa chaguo la Ukawa na kwamba kinachofanyika sasa ni kutekeleza taratibu na kanuni za kikatiba za vyama hivyo kabla ya kutambulisha rasmi Ilani ya yao na kumkabidhi jukumu mgombea wao mteule.

BASATA Yamfungia Shilole Kutojihusisha Na Muziki Mwaka Mmoja
Dkt Slaa Akanusha Yaliyosambaa Kuhusu Yeye, Lowassa Na Chadema