Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye pamoja na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad wanatarajiwa kung’arisha jukwaa la mashabiki wa Simba na Yanga katika mechi ya watani hao wa jadi itakayofanyika Oktoba Mosi mwaka huu.

Hatua hiyo imekuja kufuatia maombi ya Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) kuwaomba viongozi hao kuhudhuria mtanange huo wa kukata na mundu katika Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL 2016/17), utakaopigwa jijini Dar es Salaam.

Katibu Mwenezi wa Bavicha, Edward Simbeye amesema kuwa wamepata taarifa za awali kuwa Lowassa amekubali kuhudhuria mechi hiyo lakini itawezekana endapo mazungumzo kati ya viongozi wa dini na upande wa Serikali yatafanikiwa kuzima mpango wa Chadema kuitisha maandamano na mikutano nchi nzima siku hiyo.

“Ni kweli tulimuomba Lowassa awe miongoni mwa mashabiki watakaohudhuria pambano hilo na kwa taarifa za awali amekubali,” Simbeye anakaririwa.

Aliongeza kuwa Lowassa ataambatana na viongozi wengine wa Ukawa akiwemo Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR –Mageuzi, James Mbatia na Mwanasheria wa Chadema, Tundu lissu.

Simba wataingia uwanjani kwa lengo la kuusaka ushindi ikiwa ni pamoja na kupooza machungu ya kufungwa mara mbili na Yanga katika msimu uliopita.

Video: Walichokisema Magic FM baada ya kutakiwa kumuomba radhi Rais JPM, Watanzania
Video: Hotuba ya Waziri mkuu Bungeni Dodoma, ahusisha mambo makuu 10