Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa ameeleza sababu zinazomfanya abaki ndani ya chama hicho, tangu alipojiunga mwaka 2015.

Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani amesema kuwa hana mpango wa kukihama chama hicho kwa sababu hana hoja na sababu za msingi za kuwaeleza watu zaidi ya millioni 6 waliomuunga mkono katika uchaguzi mkuu uliopita.

“Watu wale zaidi ya milioni sita ambazo ni kura walizozikubali Tume ya Uchaguzi. Ninawaambia nini watu wale zaidi ya milioni sita. Ninawaambia naondoka Chadema kwa sababu gani? Na kwa hoja zipi?” Lowassa ameiambia Mwananchi.

Amesisitiza kuwa hana mpango wa kuhama Chadema na hajafikiria kufanya hivyo, kwani ndicho chama kilichomuunga mkono na kuzunguka nchi nzima kumnadi akiwania nafasi ya Urais.

“Ningependa kuweka wazi kwa Watanzania kuwa sina mpango wa kuondoka Chadema hata kidogo, sijapanga wala sijafikiria kuondoka Chadema,” amesisitiza mwanasiasa huyo mkongwe.

Msimamo huo wa Lowassa umekuja ikiwa ni siku chache tangu Chadema kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu wake, upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu kumtaka mwanasiasa huyo kuweka wazi msimamo wake kwa wananchi kutokana na namna alivyokuwa akisifiwa na viongozi waandamizi wa CCM.

Lowassa amekuwa akisisitiza kuwa amefunga pingu na Chadema na kwamba anajisikia amani tangu alipojiunga na chama hicho.

Mwenyekiti wa CCM, Dkt. John Magufuli ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho tawala, Dkt. Bashiru Ally kwa nyakati tofauti wamesikika wakimsifia Lowassa kuwa ni mstaarabu anayefanya siasa safi na ‘hapigi kelele’ kam wafanyavyo watu wa chama chake.

Lowassa amewahi kueleza kuwa alishawishiwa na Rais Magufuli kurejea CCM walipokutana Ikulu, lakini aliweka msimamo wake kuwa ‘uamuzi wake haukuwa wa kubahatisha.’

Lowassa alihamia Chadema siku chache baada ya Kamati Kuu ya CCM kukata jina lake katika mchakato wa kuwania nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2015. Alipewa nafasi ya kugombea urais kupitia Chadema na kuleta ushindani mkubwa katika historia ya vyama vingi nchini, akiwa chini ya muungano wa vyama vinne vya upinzani vilivyounda Ukawa.

Ni kesho: Je, umeshampigia kura Queen Elizabeth kuwa Miss World 2018?
Makala: Diane, mtoto wa mfadhili wa ‘Kagame’ aliyegeuka mwiba kwa Serikali