Baadhi ya wananchi waliofuatilia uzinduzi wa kampeni za Ukawa uliofanyika jana katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam wameonesha kutoridhishwa na hotuba aliyoitoa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

Baadhi ya wananchi hao walionesha kutoridhishwa na hotuba fupi ya takribani dakika 10 iliyotolewa na mgombea huyo wa urais wakati ambapo maelfu walikuwa na kiu ya kumsikiliza akieleza kwa kina kuhusu ilani ya uchaguzi ya chama chake na kile alichopanga kulifanyia taifa.

“Ingawa najua kabisa kuwa uongozi mzuri haupimwi kwa kuongea maneno mengi, lakini kama leo wangeweka kuongea sana kama kigezo cha urais, mimi ni mwalimu na hapa moyoni najua Lowassa ningempa ngapi,” alisema mhadhiri wa masomo ya sheria Chuo Kikuu Cha Mzumbe, ambaye hakutaka jina lake litajwe na siku zote anamuunga mkono Lowassa..

Katika hatua nyingine, baadhi ya wananchi wameoenesha kutoridhishwa na kile walichokiita ‘summary’ iliyotolewa na mgombea huyo kwa kutaja elimu, kilimo cha kisasa, ujenzi wa reli ya kati bila kutoa ufafanuzi. Zaidi ahadi yake ya kutoa elimu bure kwa kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu ambayo hakuitolea ufafanuzi.

“Elimu itakuwa bure kuanzia darasa la kwanza hadi cho kikuu. Mtu asiniulize ntapata wapi fedha, nchi hii inalasirimali nyingi sana,” alisema Edward Lowassa.

“Lowassa ametuangusha kwa kweli, bado nilikuwa na kiu ya kumsiliza, unajua nilijua ataongelea pia tuhuma za Richmond na mengine,”alisema mwanachama mmoja wa Chadema. “Kama muda ulikuwa tatizo, kwanini waliwapa nafasi zaidi watu wengine?” aliuliza.

Ukawa

“Unajua Lowassa alipokuwa waziri mkuu alifanya mambo mengi sana, alitembelea miradi hadi ile midogomidogo na kama unakumbuka aliwashughulikia hadi wenyeviti wa mitaa uso kwa uso, hayo CCM wameyasahau wanaongelea tu Richmond, sasa Lowassa ilibidi awakumbushe watanzania CV yake hiyo kubwa,” alisisitiza mwananchi huyo anaeunga mkono Ukawa ambaye hata hivyo aliapa kutoacha kumuunga mkono Lowassa akidai kuongea sio kigezo cha utendaji na kuchukua maamuzi.

Edward Lowassa na timu nzima ya Ukawa walimaliza kwa amani uzinduzi wa kampeni zao zilizofana katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, kampeni zilizoisha majira ya saa kumi na moja na dakika 55. Timu hiyo imepanga kuelekea mikoani kufanya kampeni hizo ambapo leo watakuwa Iringa.

 

ACT- Wazalendo Kuzindua Kampeni Zake Leo
Sumaye Amjibia Lowassa, Ageuka Mwimba Kwa CCM