Vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, hatimaye jana vilifanya uzinduzi wa kampeni zake za urais katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam, mkutano ambao ulivuta maelfu ya wawananchi ukidaiwa kuvunja rekodi ya mahudhurio.

Akizungumza na wananchi waliofurika uwanjani hapo, mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa alitaja vipaumbele vilivyoko kwenye ilani ya uchaguzi ya chama hicho na kueleza kuwa kipaumbele cha kwanza ni elimu.

“Kipaumble cha kwanza katika ilani ni elimu, cha pili ni elimu na cha tatu ni elimu,” alisema Lowassa na kuongeza kuwa serikali yake itatoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu.

“Msiniulize fedha [ya kusomesha hadi chuo kikuu] nitaipata wapi. Hii nchi ina rasilimali nyingi sana na vyanzo vingi vya mapato,” aliongeza.

Ahadi hiyo ya Lowassa imeipiku ahadi ya mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli ambaye aliahidi kuwa serikali yake itatoa elimu ya bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.

Lowassa umati

Lowassa alitaja vipaumbele vingine katika ilani ya Chadema kuwa ni ujenzi wa reli ya kati, kufufua shirika la ndege nchini (Air Tanzania) na kuweka miundombinu ya kisasa ya kilimo nchini.

Katika hatua nyingine, Lowassa aliwaeleza wananchi kuwa serikali yake itafuatilia kesi za mashehe waliowekwa kizuizini visiwani Zanzibar, Babu Seya na wanae pamoja na alipo Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania, Bilali ambaye kifo chake kilitangazwa miezi michache baada ya sakata la EPA.

Aliwataka wananchi waliokuwa wakimshangilia kuwa ‘rais… rais… rais…’ kuwa wahakikishe wampigie kura kwa wingi ili aweze kushinda kweli na kuwa rais wa Tanzania.

Sumaye Amjibia Lowassa, Ageuka Mwimba Kwa CCM
CCM Wamnyemelea Lowassa Dakika Za Mwisho