Katika nchi ya kusadikika, hujazwa vitu ambavyo wananchi wa kawaida wangependa kuviona na kuvisikia vikitokea katika nchi zao.

Kwa bahati mbaya, licha ya kuwa nchi ambayo ni bora zaidi inayokidha matakwa ya wananchi wake na kuwamalizia shida zao zote au labda hata kujibu maswali yao kwa vitendo, nchi hii nzuri ya kusadikika huundwa kwa mawazo ya kufikirika tu.

Nimeanza na utangulizi huo kwa kuchukulia mawazo ya baadhi ya watanzania ambao wanatamani vitu fulani vitokee au vizungumzwe na wanasiasa katika nchi halisi ya Tanzania lakini hawayasikii.

Kati ya mambo ambayo wananchi wangependa kuyasikia kwenye mikutano ya hadhara ya Ukawa ni pamoja kusikia sauti ya mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa akisema, “Nitakapoingia ikulu nitahakikisha napamba na ufisadi kwa nguvu zangu zote kwa kasi ya ajabu”.

Wananchi wanaoishi katika nchi ya kusadikika wanapenda kusikia hilo kwa kuwa kwa asilimia kubwa suala hilo limekuwa ajenda kuu ya wapinzani wao (CCM) huku wakitumia kila mbinu kuwaaminisha watanzania kuwa Lowassa ni fisadi na kwamba atakapoingia madarakani ataendeleza ufisadi kwa kiasi kikubwa.

“Kama alikuwa waziri mkuu kwa miaka miwili tu akaiba bilioni 4, akiingia ikulu itakuwaje,” namkariri mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, Samuel Sitta.

Naye mgombea wa CCM ameonekana kutumia nguvu kubwa kueleza jinsi ambavyo atapambana na ufisadi nchini ikiwa ni pamoja na kuunda mahakama maalum ya kushughulikia ufisadi.

“Nitaanzisha mahakama maalum za kushughulikia ufisadi ili majizi na mafisadi ya nchi hii yaweze kufungwa haraka,” anasema Magufuli karibu kila anapopita.

Ingawa inawezekana wakawa wanatumia kete hiyo kisiasa, ukweli ni kwamba ufisadi ni tatizo kubwa sana nchini hivi sasa na limekuwa likilitafuna taifa letu kwa muda mrefu. Tumekuwa tukisikia mabilioni yakiibiwa kwenye masakata ya Richmond, EPA, ESCROW na mengine mengi.

Lowassa na umati

Kwa kuwa hoja hiyo ya kupambana na ufisadi ilikuwa hoja kuu ya Chadema kwa miaka mingi, ni dhahiri kuwa hoja hiyo imehamia upande wa CCM ghafla huku mratibu wa hoja hiyo pia (Dk Wilbroad Slaa) akiripotiwa kuongeza nguvu upande huo ambao alikuwa anaushambulia kila siku.

“Serikali ya CCM ni serikali ya kifisadi,” alikuwa akisema Dk Slaa.

Hivyo watanzania wengi wanaoishi kwenye nchi halisi wangependa kusikia sauti ya rais mtarajiwa kwa tiketi ya Chadema akizungumzia mikakati yake ya kuzuia wizi na ufisadi kwa sauti yake mwenyewe.

Ingawa wapinzani wake wameligeuza sakata la Richmond kama silaha zaidi ya kumpooza Edward Lowassa asiwe na ajenda ya kupambana na ufisadi, ukweli bado una baki palepale kuwa wagombea hao wa Chadema na CCM wote wamewahi kuhusishwa katika masakaata ya ufisadi kwa nyakati tofauti.

Baadhi ya wananchi tayari wameulewa utetezi wa Lowassa anayeshambuliwa kwa kila mbinu kupitia kashfa ya Richmond ya mwaka 2008, hata waliohusika kwenye kashfa za hivi karibuni ambazo ni rahisi zaidi kuyakumbuka kutokana na ubichi wake, sasa hivi wamepumzishwa. Lakini vidole vyote hivi sasa ni kwa Lowassa.

Sisi wananchi wa nchi ya kusadikika, tunaota kuwa Edward Lowassa ametangaza kupambana na ufisadi kwa nguvu zote atakapoingia ikulu kwa sababu tunaamini anaweza. Tunamkumbuka Lowassa alipokuwa waziri mkuu alikuwa na uwezo wa kuwasimamisha mara moja watendaji waliodaiwa kuhujumu miradi mbalimbali hadi katika ngazi za kijiji.

Tunakumbuka uamuzi wake wa kuvunja mkataba wa maji ambao ungeligharimu taifa. Hivyo tunaamini kabisa kuwa anaweza kupambana na ufisadi.

Ni kweli kabisa tunahitaji mabadiliko, yanaweza kuwa nje ya CCM, asante kwa kipaumbele muhimu cha elimu bure hadi chuo kikuu, na kweli hayo ni mabadiliko makubwa sana na hajawahi kutokea nchini, ila usiache nyuma vita dhidi ya ufisadi.

Ombi letu kwako Lowassa sisi wananchi wan chi ya kusadikika, ifanye ndoto yetu kweli, weka mapambano dhidi ya ufisadi kuwa moja kati ya makubwa utakayoyafanya, tunaamini unaweza kwa vitendo tena kwa kasi ambayo haijawahi kutokea.

 

 

 

 

 

 

 

Zlatan: Nipo Tayari Kwa Lolote
Kuziona Stars Na Super Eagles Tsh 7000