Mwenyekiti wa Chama Cha Wanachi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa atafanya ziara yake muda mfupi ujao itakayofuta kile alichokiita propaganda za Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Maalim Seif Sharif Hamad.

Profesa Lipumba amesema kuwa ahadi anazozitoa Zitto kuwa viongozi wengine wa juu wa CUF watajiunga na ACT-Wazalendo ni propaganda zisizo na ukweli.

Mwanasiasa huyo amedai kuwa hata idadi ya viongozi wa ngazi mbalimbali anazozitaja Zitto kuwa wamejiunga na ACT Wazalendo sio za kweli, hali aliyodai ni kutaka kuonesha umma kuwa CUF wamefutika visiwani humo.

Aidha, Profesa Lipumba ameeleza kuwa hivi punde ataanza ziara yake visiwani humo na ukweli utajidhihirisha kuwa bado CUF ina nguvu.

“Sio  kweli wanavyosema kuwa asilimia 90 ya viongozi wa matawi ya CUF wamehamia ACT. Hizo ni propaganda za Maalim Seif. Waliojiunga CUF ni viongozi wa chama katika ngazi mbalimbali na sio wanachama wa kawaida ambao naamini wako wengi kuliko waliotoka,” Mwananchi wanamnukuu Profesa Lipumba.

“Tunajipanga na tutakwenda kuzungumza na wanachama na tutakuwa na mpango mkakati maalum wa kuimarisha CUF kuhakikisha inakuwa imara Pemba na Unguja. Lengo ni kuleta umoja wa kitaifa na kuondoa uongo wa Seif,” aliongeza.

Maalim Seif ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa CUF kabla ya kufukuzwa na Profesa Lipumba, alijiunga na ACT-Wazalendo Machi 18 mwaka huu. Kwa mujibu wa Zitto, viongozi wa matawi 675 wameshusha bendera za CUF an kupandisha za ACT Wazalendo huku wengine wakisubiri kupata bendera zaidi.

Zitto amesema viongozi wa majimbo 54, kata 101 pia waliikacha CUF na kujiunga na ACT-Wazalendo.

Live Ikulu: Rais Magufuli akizungumza na wachezaji Taifa Stars, bondia Mwakinyo
Ajinyonga muda mfupi baada ya kuandika ujumbe Facebook