Wababe wawili, Amir Khan wa Uingereza na Terrence Crawford wa Marekani usiku wa leo wanatarajia kukata mzizi wa fitna wa kumpata mbabe wa masumbwi wa uzito wa Welterweight wa ubingwa wa dunia wa Shirikisho la Masumbwi Duniani (WBO).

Terrence aka ‘The Bud’ ambaye ni bingwa wa dunia mwenye rekodi ya kushinda mapambano yake yote, atakuwa na kibarua cha kutetea taji lake dhidi ya bondia huyo kutoka Uingereza anayetumia jina la ‘King Khan’ akiwa ulingoni.

Pambano hilo litakalorushwa pia kupitia mfumo wa pay-per-view litashuhudiwa katika ukumbi maarufu wa Madison Square Garden jijini New York nchini Marekani.

Ingawa idadi kubwa ya mashabiki wanampa nafasi zaidi Terrence kutokana na uwezo wake wa kuwa na mbinu nyingi anapokuwa jukwaani, kasi ya kurusha masumbwi ya Amir Khan pamoja na uzoefu wake ni silaha inayowafanya wengi pia kuamini chochote kinaweza kutokea kwenye pambano hilo.

Terrence ambaye anatajwa kuwa katika nafasi ya pili ya ubora duniani kwa mujibu wa ‘The Ring’ anatetea taji lake kwa mara ya pili tangu alipofanikiwa kumpiga kwa KO Jeff Horn, Juni 2018.

Kwa upande wa Khan, hili ni pambano lake la kwanza la kusaka ubingwa wa dunia tangu alipopoteza kwa kupigwa KO na Canelo Alvarez mwaka 2016.

Kwa saa za Afrika Mashariki, pambano hili ambalo limetajwa kushuhudiwa leo (Aprili 20), litashuhudiwa majira ya Alfajiri ya Aprili 21.

Ajikata kidole baada ya kupigia kura chama asichokita
Mchezaji mkongwe aponda uamuzi wa Man United kuhusu Solskjaer