Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ametoa ujumbe wake akiwataarifu Watanzania kuwa amepewa adhabu ya kusimamishwa kushiriki vikao vya Bunge hadi Januari mwakani.

Lema ambaye jana alihojiwa na Kamati ya Haki, Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhusu kauli yake ya kuunga mkono kauli iliyowagharimu Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Profesa Mussa Assad kuwa ‘Bunge ni dhaifu’, leo alilimwa adhabu inayofanana na mbunge huyo mwenzake.

Lema ameandika kwenye akaunti yake ya Twitter ujumbe akieleza kuwa moyo wake una amani kutokana na adhabu aliyopewa kwani anaamini anazidi kuwa na uhusiano na haki.

“Nimesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge mpaka  January 2020.Moyo wangu una amani sana,kwani mahusiano yangu na HAKI yanaendelea kuimarika zaidi.Nawatakia Wabunge wenzangu kazi njema katika wajibu huu,sitanyamaza hata kama adhabu itakuwa ni mauti,” ametweet.

“Msiogope.Mungu aliyetupa macho sio kipofu kwamba haoni, Mungu aliyetupa masikio sio kiziwi kwamba hasikii. Yeye ni Mungu asiyekuwa na msongo wa mawazo kama sisi. Siku imekaribia sana kwa kila mtu kulipa kwa kadri alivyopanda,” ameongeza kwenye tweet nyingine.

Adhabu dhidi ya Lema ilifikiwa leo Bungeni baada ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka kusoma ripoti ya kamati na kupendekeza adhabu ya kutohudhuria mikutano mitatu, adhabu ambayo ilipitishwa na Bunge baada ya Spika Job Ndugai kuwahoji.

Wakati adhabu hiyo inatolewa, wabunge wa upinzani wakiongozwa na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe walitoka nje ya ukumbi wa bunge.

Video: Aliyempiga mabusu Beyonce mbele ya Jay Z azua balaa
Mwanamke alijifungua juu ya mti akikwepa Kimbunga Idai