Klabu ya La Galaxy imetangaza kumaliza mkataba na kiungo kutoka nchini England Steven Gerrard, baada ya kufanya nae kazi kwa kipindi cha miaka miwili.

Gerrard alijiunga na La Galaxy mwaka 2015 akitokea nchini kwao England, ambapo alimalizana na Liverpool aliyoitumikia tangu akiwa na umri mdogo.

Maamuzi ya kuondoka nchini Marekani ambapo aliamini huenda angefanya vizuri kama alivyokuwa katika ligi ya England, yanamuweka njia panda kiungo huyo ambaye ana sifa ya kipekee ndani ya klabu ya Liverpool.

Mpaka sasa Gerrard hajaweka wazi kama ataendelea kucheza soka ama kustaafu mchezo huo, jambo ambalo limeendelea kufanyiwa kazi kwa undani na baadhi ya vyombo vya habari vya nchini kwao England.

Alipohojiwa kuhusu mustakabali wake, Gerrard alisema ni mapema mno kutangaza nini atakachokiamua baada ya kuthibitishiwa hatosaini mkataba mpya na klabu ya La Galaxy.

Gerrard anaondoka La Galaxy huku akiacha kumbukumbu ya kufunga mabao manne na kutoa pasi 14 zilizozaa mabao ya klabu hiyo kwa kipindi cha misimu miwili aliyocheza soka nchini Marekani.

Gerrard anakua mchezaji wa pili kutoka nchini England kuthibitishiwa hatosaini mkataba mpya na klabu za nchini Marekani, baada ya Frank Lampard kupokea taarifa kama hizo kutoka katika uongozi wa New York City FC.

#HapoKale
Kiwanda cha Konyagi, pombe kali feki chanaswa Dar