Klabu maarufu ya nchini Marekani LA Galaxy imethibitisha taachana na beki wa kushoto kutoka England Ashley Cole, na kusisitiza itaendelea kufanya kazi na mshambuliaji kutoka Sweden Zlatan Ibrahimovic, licha ya kuhusishwa na mpango wa kutaka kurejea nchini Italia kujiunga na AC Milan.

Cole mwenye umri wa miaka 37, alisajiliwa na LA Galaxy mwaka 2016 akitokea nchini Italia alipokua akiitumikia klabu ya AS Roma, na mwaka 2017 alitangazwa kuwa nahodha wa kikosi cha wamarekani hao.

Uongozi wa klabu ya Galaxy umetoa taarifa hizo baada ya kushindwa kuafikiana na Cole masuala kadhaa ya kimkataba, na umeamua kuthibitisha suala la kuondoka kwake, itakapofika mwezi Januari mwaka 2019.

Kwa upande wa Ibrahimovic, ambaye alijiunga na LA Galaxy mwanzoni mwa mwaka huu 2018, ataendelea kuutumikia mkataba wake wa mwaka mmoja.

Mshambuliaji huyo bado anaendelea kuhusishwa na taarifa za kutakiwa na klabu ya AC Milan, lakini uongozi wa LA Galaxy haujasema chochote kuhusu tetesi hizo ambazo zinachukua kasi siku hadi siku kwenye vyombo vya habari vya barani Ulaya.

Tayari Ibrahimovic ameshaifungia Galaxy mabao 22, na ametajwa kwenye orodha ya wachezaji wanaowania tuzo ya  MVP, akishindanishwa na Miguel Almiron, Carlos Vela, Josef Martinez na mshambuliaji wa zamani wa Manchester United Wayne Rooney.

Ibrahimovic pia ametajwa kwenye kipengele cha tuzo ya mchezaji bora mgeni, akishindanishwa na Rooney na Vela.

Watumishi watakiwa kuongeza ubunifu
Sadio Mane aongeza morali Liverpool