Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zakary Kakobe ameeleza kwanini Rais John Magufuli anapaswa kupongezwa kwa ununuzi wa ndege mpya ingawa pesa zinazotumika ni kodi walizolipa wananchi.

Akizungumza leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, wakati wa mapokezi ya ndege mpya aina ya Airbus A220-300, Askofu Kakobe ameibua swali hilo na kulikamilisha kwa mfano wa rubani anayepongezwa na abiria kwa kufanikisha kutua kwa ndege iliyopita juu ya bahari kwa saa saba.

“Wengine wanasema ‘lakini hizi si kodi zetu hizi ndege, sasa sifa-sifa zote hizi za nini kwa Rais Magufuli…’,” alisema Askofu Kakobe.

“Ndege inapotoka London, Uingereza kutua New York, Marekani inapita juu ya bahari kwa saa saba. Wasafiri wengi wakitua New York wanapiga makofi na vigelegele kwa rubani. Sasa mtu mmoja akasema ‘tunampigia makofi rubani wakati tumelipa nauli, ya nini?’. Ndivyo ilivyo sasa hivi. Tumelipa kodi zetu kweli lakini tunaye rubani Rais John Pombe Magufuli,” aliongeza.

Askofu Kakobe alieleza kuwa anakubali kazi anayoifanya Rais Magufuli akieleza kuwa anastahili heshima zote.

Viongozi mbalimbali wa dini pamoja na viongozi wa Serikali na wananchi kwa ujumla wameungana na Rais Magufuli kupokea ndege hiyo mpya ikiwa ni wiki chache tangu ndege nyingine ya aina hiyo kuwasili nchini.

LIVE: Rais Magufuli akihutubia baada ya ndege nyingine ya Tanzania kuwasili
WhatsApp yaanza majaribio ya kutumia 'Fingerprint' kama nywira

Comments

comments