Na Josefly:

Leo , Mei 21 ni kumbukizi ya miaka 23 ya tukio la majonzi na simanzi lililoikumba Tanzania na Dunia kwa ujumla. Siku kama ya leo mwaka 1996, ni tarehe yenye rangi nyekundu kwenye kalenda ya mioyo ya watu wengi.

Ilikuwa siku ya Jumanne ambayo rangi ya maji ya Ziwa Victoria iliyozoeleka kuwa ile iliyoakisi uzuri wa rangi ya mawingu ilifyonza wekundu wa damu ya Watanzania na raia wa nchi nyingine, zaidi ya 894 waliopoteza maisha baada ya meli ya MV Bukoba kuzama ndani ya ziwa hilo.

MV Bukoba, meli iliyoundwa mwaka 1979, ililazimishwa kubeba mzigo isioumudu ikiwa kwenye Bandari ya Bukoba. Watendaji waliojaa tamaa ya kuingiza pesa nyingi waliishindilia mizigo rundo na abiria bila kujali uwezo wake wa kubeba. Kwa kawaida, meli hiyo ilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 430 tu, lakini ilishindiliwa idadi ya abiria ambayo hata vitabu vya kumbukumbu vilishindwa kutoa picha halisi ya idadi.

Hebu fikiria, kama waliopoteza maisha tu walikuwa 894 ndani ya meli iliyokuwa na uwezo wa kubeba abiria 430 tu, na kwa neema ya Mungu wapo wengi waliosalimika!

Vitabu vya kumbukumbu vya safari ya mwisho ya meli hiyo vilionesha kuwa jumla ya watu 443 walipanda kwenye daraja la kwanza na la pili pekee. Daraja la tatu ambalo ni la wengi zaidi halikuonesha idadi. Yaani upigaji wa tiketi za holela, tamaa ya vijisenti iliwafunika macho watendaji wakasahau thamani ya maisha, wakawarundika abiria. Wakashindilia mizigo kila penye nafasi bila kujali kuwa kikomo cha mizigo kilipaswa kuwa tani 850 tu.

Punda akielemewa na mzigo hulala chini, lakini bakora za nahodha wa meli ile, bila shaka baada ya kukabidhiwa ‘mshiko’ zilihakikisha MV Bukoba inaamka na mzigo ilimradi tu ivuke ng’ambo!

“Bora punda afe mzigo ufike,” msemo huu wa kikora ulishindwa, punda aliteketea na alichobebeshwa.

Meli ile ilianza kwa kujikongoja, ikatoa milio ya kila aina ya kuzidiwa. Ikaanza kuiaga bandari ya Bukoba ikihangaika iwezevyo. Wapo waliochelewa safari, wakaiona inavyoondoka na wakaumia, walitamani kuwa sehemu ya safari! Lakini, hakuna aliyeisikia sauti ya kilio cha meli ile.

Ilijikongoja hadi ilipoiona ng’ambo. Ilipobakiza Kilometa 50 kutoka katikati ya kitovu cha jiji la Mwanza na mita chache tu za umbali wa maji ya ziwa, ilishindwa kuendelea.

Kama ilivyo kwa punda anapozidiwa, ililala. Vilio vikaanza kusikika, meli ile ikaanza kuzama taratibu. Na hapo ndipo maisha ya Watanzania wengi pamoja na raia wa kigeni yalipoishia.  Karibu kila kaya ilikuwa na msiba, kama sio wa ndugu au jamaa basi ni wa rafiki.

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa akatangaza siku tatu za maombolezo. Lakini hakuwaacha wale wapiga dili waliosababisha msiba huu mkubwa kwa uzembe wa hali ya juu. Maafisa tisa wa Shirika la Reli kitengo cha Majini pamoja na nahodha wa meli hiyo walikamatwa na kuburuzwa mahakamani.

Timu ya waokoaji, wengine kutoka Afrika Kusini iliingia kazini kusaidia. Ndani ya siku kadhaa kuna watu walikuwa bado wako hai ndani ya meli lakini uwezekano wa kuwafikia ulikuwa mtihani. Baada ya kuhangaika, waliamua kutoboa meli hiyo ili kuingia ndani, na hapo mambo yalikuwa tofauti zaidi. MV Bukoba ikazama yote ndani na kuacha ncha yenye jina lake ikiiaga dunia. Kweli mwendo iliupiga lakini haikuwa na nguvu ya ziada.

Baadhi ya watu waliokolewa. Lakini zoezi kubwa lilikuwa kuiokoa miili ya abiria. Miili hiyo ilizikwa kwenye makaburi ya pamoja katika eneo la Nyakato jijini Mwanza. Tanzania, hasa mikoa ya Kanda ya Ziwa ilipigwa ubaridi wa majonzi mazito na sauti za vilio vilisikika kila kona.

Mmoja kati ya watu maarufu ambao wanaguswa moja kwa moja na tukio hili, ni mrembo Flavian Matata ambaye mwaka 2013 alitajwa na Jarida la Forbes kwa kuingiza ukwasi mrefu. Pia, mwaka 2017 jarida la kimataifa la okay.com lilimtaja kuwa miongoni mwa wanawake 100 bora zaidi Afrika. Flavian alimpoteza mama yake mzazi.

Sio Watanzania peke yake waliopoteza maisha. Watu wengi wema walipoteza maisha, lakini pia wenye nia mbaya nao walikuwemo. Kundi la Kigaidi la Al-Qaeda lilitangaza kuwa kamanda wake aliyekuwa anashika nafasi ya pili ya uongozi wa kundi hilo baada ya Osama Bin Laden, Abu Ubaidah al-Banshiri naye alipoteza maisha kwenye ajali hiyo! Alifuata nini Bukoba? Hakuna anayejua! Yeye alikuwa anaishi jijini Nairobi nchini Kenya, akawa anajidai kuwa mfanyabiashara na alimuoa raia wa Kenya.

Uchunguzi wa tukio hilo ambao uliandikwa pia na Nahodha Mkenya, Joseph Muguthi kwenye gazeti la Daily Nation, ulitaja sababu za kuzama kwa meli hiyo na kutookolewa kwa abiria wengi kuwa ni pamoja na kukosekana kwa vifaa vya uokoaji vya kutosha kama ‘life jackets’, vifaa vilivyokuwepo havikuwa vinakaguliwa mara kwa mara, kuzidisha mizigo kupita kiasi na wafanyakazi wengi wa kiufundi wa meli hiyo hawakuwa na leseni ya kufanya kazi hiyo.

Nahodha Muguthi pia alieleza kwenye Makala yake kuwa kitengo cha usafirishaji wa majini kilijaa watumishi ambao hawakuwa na elimu ya usafiri wa majini hususan safari za meli.

Msiba huu mzito uliikumbusha dunia kuzama kwa meli ya Titanic, Aprili 14 mwaka 1912 majira ya saa tano usiku na kusababisha vifo vya watu 2,224. Ilikuwa ikitokea Southampton nchini Uingereza kwenda New York Marekani.

Tunapaswa kuhakikisha tunachukua kila hatua kuepuka ajali zinazosababishwa na uzembe na tamaa, zinazotugharimu maisha.

Mungu azilaze mahali pema roho za ndugu zetu waliopoteza maisha kwenye ajali hii mbaya.

Video: Hii ndiyo adhabu utakayopata ukikutwa na mfuko wa plastiki
Mtoto wa Ruge apata shavu kwa Nandy ''Tupo juu kila siku''