Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea ambaye yeye pamoja na Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu leo wamechomwa na joto la Kamati Kuu ya Chadema, ameeleza uhusiano wake na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Akizungumza muda mfupi baada ya Kamati Kuu kuwavua vyeo vyote ndani ya chama hicho kasoro Ubunge kutokana na sauti zao zilizosambaa mitandaoni wakisikika kupanga mbinu hasi dhidi ya Meya huyo, Kubenea amedai kuwa hana tatizo naye na kwamba ndiye rafiki yake wa karibu zaidi.

‘Kila binadamu ana rafiki yake wa karibu, na rafiki yangu wa karibu ni Boniface Jacob,” Kubenea amesema.

Akizungumzia sauti zao dhidi ya Meya Jacob, Komu alisema kuwa walikuwa ndani ya gari wakizungumzia mambo mengi na kwamba mazungumzo hayo yaliingia katikati ya mambo mengine.

“Hakuna hujuma yoyote ambayo tulikuwa tumeipanga, tulikuwa tuna mazungumzo mengine na hayo yakaingilia kati,” alisema Komu.

Akizungumzia uamuzi wa kamati kuu ya chama hicho, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, John Mnyika, alisema kuwa wabunge hao mbali na kuvuliwa nyadhifa zote kasoro ubunge, wanatakiwa kuandika barua ya kuomba radhi.

Aidha, Kubenea aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye yuko imara na kwamba hana mpango wa kuhama chama hicho kikuu cha upinzani.

“Mimi niko imara mno, ningekuwa legelege nisingeenda mbele ya Kamati Kuu, uthibitisho wa kwenda mbele ya kamati kuu na kupitia vigingi vyote hivyo ni wazi kuwa mimi ni imara. Waambieni CCM mimi ni imara hawaniwezi,” alisema Kubenea.

Diddy, Cassie wapigana chini
Mwana FA, Richie wateuliwa kuwa wajumbe Bodi ya BASATA