Korea Kaskazini wamezungumzia sababu za kuvunjika kwa mkutano kati ya Rais Donald Trump na Kiongozi wake, Kim Jong Un mapema jana jijini Honai nchini Vietnam, wakipinga sababu zilizotolewa na Rais huyo.

Jana, Trump alisema kuwa alishindwa kuendelea na kikao chao kwa sababu Korea Kaskazini ilitaka vikwazo vyote dhidi yake viondolewe na kwamba waliahidi kuharibu baadhi ya sehemu ya vinu vya nyuklia. Hatua ambayo alisema Marekani haikuwa imejiandaa kuifikia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, Ri Yong-ho alisema kuwa hawakutaka vikwazo vyote viondolewe wakati huu, bali waliomba baadhi ya vikwazo ambavyo vinadhoofisha moja kwa moja hali ya uchumi wa wananchi wake viondolewe.

Aliongeza kuwa nchi yake iliahidi kuachana na zoezi la kufanya majaribio ya mabomu ya kinyuklia pamoja na kuharibu vinu vya makombora hayo, lakini Marekani waliikosa shabaha muhimu siku hiyo.

“Wameikosa shabaha muhimu na fursa ya siku hiyo. Sidhani kama fursa ya mkutano kama ile itatokea tena hivi karibuni. Msimamo wetu utabaki palepale na mapendekezo yetu hayatabadilika daima, hata kama Marekani itapendekeza kufanyika kwa mazungumzo mengine,” Ri aliwaambia waandishi wa habari.

China ambayo ni mshirika mkubwa wa Korea Kaskazini imeeleza kuwa ina imani majadiliano kati ya pande hizo mbili yatafanyika tena ili kufikia muafaka wa kuondoa taharuki iliyokuwepo.

BASATA wamshushia Dudu Baya nyundo nyingine nzito
Marekani yatoa zawadi ya mabilioni kumnasa mtoto wa Osama