Kiungo mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Luis Miquissone amesema ameanza kujiandaa na kujipanga kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu pamoja na michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Akizungumza baada ya kuwasili jijini Dar es salaam sambamba na wachezaji wenzake wakitokea mjini Sumbawanga mkoani Rukwa wakipitia Mbeya, kiungo huyo kutoka Msumbiji amesema amefurahi kuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kilichopata mafanikio makubwa msimu wa 2019/20.

Amesema shughuli kubwa iliyo mbele yake kwa sasa ni kuhakikisha anajipanga na kujiandaa kikamilifu kwa msimu mpya wa michuano ya Tanzania na ile ya kimataifa, ambapo klabu yake itashiriki Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

“Najihisi vizuri kuona timu yangu imepata kombe lingine la Shirikisho, sina budi kumshukuru Mungu kutokana na ushindi aliotupa, sasa hivi ninajipanga na kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao pamoja na mashindano ya kimataifa,” alisema Luis.

Amesema siri ya mafanikio ya klabu yake ya Simba SC ni kufuata kwa makini maelekezo ya kocha wao Sven pamoja na benchi zima la ufundi huku kila mchezaji akiamini uwezo wa mwenzake na kucheza kitimu wakati wote.

“Kufuata maelekezo ya kocha wetu ndio nguzo pamoja na ushirikiano tuliokuwa nao sisi wenyewe wachezaji, vile vile tunawashukuru mashabiki wetu kwa ushirikiano wao,” amesema kiungo huyo aliejiunga na Simba SC wakati wa dirisha dogo mwanzoni mwa mwaka huu akitokea UD Songo ya nchini kwao Msumbuji.

Miquissone alifunga bao la kwanza dhidi ya Namungo FC wakati wa mchezo wa fainali Kombe la Shirikisho Tanzania bara uliochezwa Jumapili mjini Sumbawanga, kabla ya nahodha na mshambuliaji John Rafael Bocco hajafunga bao la pili, huku bao la wapinzani likifungwa na Edward Charles Manyama.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Agosti 5, 2020
Willian, Chelsea bado ngoma mbichi