Kiungo mshambuliaji wa Klabu ya Arsenal, Mesut Ozil amebadili hali ya hewa ya vichwa vya habari vilivyomuandama hivi karibuni, baada ya kuonesha kiwango cha juu dhidi ya Burnley katika uwanja wa nyumbani.

Mchezaji mwenzake, Sead Kolasinac amesema kuwa kiwango alichokionesha Ozil ambaye anasadikika kuwa kati ya wachezaji bora zaidi wa soka duniani hivi sasa, kilitosha kuwanyamazisha wakosoaji wake baada ya kikosi alichokiongoza kugawa kipigo cha 3-1 dhidi ya Burnley.

Kocha wa Washika Bunduki hao, Unai Emery pia alimpa nafasi kubwa Ozil akimfunga kitambaa cha unahodha kwa mara ya tano kwenye msimu. Baada ya mchezo huo, Emery alisisitiza kuwa Ozil mwenye umri wa miaka 30 ana maisha marefu ndani ya viunga vya Emirates.

Kolasinac ameeleza kuwa wachezaji na uongozi wa Arsenal wako nyuma ya Ozil kwa kila jambo hasa katika kipindi cha misukosuko.

“Hivyo ndivyo inavyokuwa unapokuwa mkubwa kama Mesut [Ozil] alivyo. Kwa kawaida kunakuwa na vichwa vya habari hasi lakini sisi kama timu hatuvipi nafasi, na hata Mesut pia havipi nafasi,” alisema.

“Hicho ndicho kitu muhimu. Tuko nyuma ya Meust, wafanyakazi wote na wachezaji wote. Vitu hasi vinaandikwa, lakini hayo ndiyo hutokea. Katika maisha, sio kila kitu kitakuwa chanya-wakati mwingine kuna mambo hasi huandikwa kuhusu wewe pia. Lakini kiwango chake kimewanyamazisha wakosoaji wake,” aliongeza.

Arsenal inaendelea kupambana, ikishika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi kwa alama 37, alama 11 nyuma ya Liverpool iliyojikita kileleni.

TFF yapata msiba, kiongozi wake aaga dunia
Japan yapata pigo kuporomoka kwa idadi ya watu, watoto