Meneja wa klabu ya Southampton, Ronald Koeman ametangaza msimamo wa kutokua tayari kumuachia mshambuliaji kutoka nchini Senegal, Sadio Mané ambaye anawindwa na klabu ya Man Utd.

Koeman, amesisitiza msimamo huo alipozungumza na vyombo vya habari baada ya tetesi za usajili wa mshambuliaji huyo kuchukua nafasi kubwa hapo jana, ambapo amesema hayupo tayari kuona kikosi chake kikibomolewa tena kwa sasa.

Meneja huyo kutoka nchini Uholanzi amesema lengo alilonalo kwa sasa ni kutaka kutimiza mipango aliyojiwekea kwa wachezaji wake wote alionao katika msimu huu, baada ya msimu uliopita kushindwa kutinga kwenye nne bora na kupata nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Hata hivyo Koeman, amesema mpaka sasa hakuna ofa yoyote iliyotumwa klabuni hapo, hivyo hatopenda kulizungumzia suala hilo tena, na kama atapokea ombi la kusajiliwa kwa Mane hadhani kama atalikubali kutokana na msimamo alioutangaza.

Man Utd waliripotiwa kuwa katika mipango ya kutaka kumsajili Mane, baada ya kuvurugiwa mikakati ya kumsajili mshambuliaji kutoka nchini Hispania, Pedro Rodrigues ambaye amebadili muelekeo kwa kujiunga na Chelsea.

Polisi: Marufuku Kuwazomea Waliovaa Sare Za Chama
Mrema Akiri Nguvu Ya Lowassa Ni Zaidi Yake Mwaka 1995