Klabu ya Yanga kupitia kwa mwenyekiti wake Mshindo Msolla imetoa siku nne kwa wale wote wanaotumia nembo ya klabu kujinufaisha.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa wote wanaotengeneza jezi na vifaa vingine vya michezo waache mara moja.

Amesema kuwa itakapofika tarehe 30 mwezi huu, mtu yeyote atakayejihusisha na uuzaji wa jezi feki hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

”Tunatoa siku nne, wote wawe wamejisalimisha na lengo la kuwaita watu hao wanaojihusisha na uuzaji wa jezi ni kufanya nao mazungumzo kujua ni namna gani wanaweza kusaidiana kwenye suala hilo la mauzo ya jezi na vifaa mbalimbali vyenye nembo ya klabu,”amesema Msolla

Aidha ameongeza kuwa, tarehe 27/07 kutakuwa na matukio matatu, moja ni kutambulisha jezi, pili kutambulisha wachezaji wapya na tatu ni mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

Pia amesema usajili wao umezingatia matakwa ya kocha mkuu Mwinyi Zahera, huku akisema wamesajili kulingana na matakwa ya mwalimu, hata huko alipo lazima atakuwa anafuraha maana wachezaji wote wa nje na ndani aliokuwa akiwahitaji wamepatikana pia siku tatu zilizopita mwalimu alituma program ya mazoezi.

 

Video: Jua halinichoshi, Naamka alfajiri | Mama anayezungusha mboga Mtaani kwenye beseni
LIVE: Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia Bunge