Mwenyekiti wa matawi ya klabu ya Young Africans nchini kote Bakili Makele ameushutumu uongozi wa shirikisho la soka nchini TFF kwa kushindwa kutoa ushirikiano, wakati wa safari ya kikosi chao ya kuelekea mjini Algers nchini Algeria kwa ajili ya mchezo wa mzunguuko wa kwanza hatua ya makundi, kombe la shirikisho la soka barani Afrika CAF.

Makele amesema TFF wameshindwa kutimiza jukumu lao la kumtuma muwakilishi wao katika msafara wa kikosi cha Young Africans ambao ulisafariki juma lililopita na kurejea jana mchana kupitia Mashariki ya kati.

Amesema jambo hilo limemsikitisha kama kiongozi wa matawi yote ya Young Africans, na anaamini hata kwa wanachama wengine litakua limewasikitisha kutokana na jukumu hilo kuwa katika uwezo wao.

Wakati huo huo Bakili Makele wameutaka uongozi wa shirikisho la soka nchini TFF kurejesha fedha wanazowadai ili kufanikisha shughuli za uendeshaji wa klabu hiyo ambayo kwa sasa haipo vizuri kiuchumi.

Kiongozi huyo ameeleza kuwa TFF iliwakata Young Africans zaidi ya shilingi milioni 200 kupitia VAT baada ya kuingiza mashabiki bure katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe.

Young Africans iliingiza mashabiki bure wakati huo ikiwa chini ya Mwenyekiti wake, Yusuph Manji, ambaye alilipia gharama zote za tiketi Juni 18 2016 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Makele ameutupia lawama uongozi wa TFF akisema kuwa wamekuwa wakiwanyanyasa ilihali wanajua klabu inapitia wakati mgumu hivi sasa haswa katika suala la kuyumba kiuchumi.

“Kama TFF au Bodi ya ligi inatudai chochote ikate kwenye hela tunayowadai lakini sio kuzuia mapato yetu kwa sasa tupo kwenye hali ngumu.

“Sio siri kwa sasa tumeyumba kichumi na tuna hali mbaya kwahiyo TFF iache kuzuia mapato yetu ya uwanjani,” alisema Bakili.

Mbali na fedha za mdhamini, Makele amefunguka pia kuhusiana na kutopokea vifaa vya CAF kwa ajili ya mashindano ya kimataifa kwa kuilaumu TFF kuwa inahusika kwa maana vinapitia kwao.

Kiongozi huyo wa matawi amewaomba TFF chini ya Rais Wallace Karia, wabadilike na warejee katika usahihi wa uwajibikaji ili walitendee haki soka la Tanzania wakiwa kama mlezi mkuu.

Mwadini Ally awazidi kete Sure Boy, Frank Domayo
Wallace Karia awaaga vijana wa TSC