Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ameituhumu Marekani kuwa ilikuwa na nia isiyo njema wakati wa mkutano kati yake na Rais Donald Trump nchini Vietnam.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Korea (KCNA), Kim Jong Un ameyasema hayo Alhamisi hii alipokutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Alisema kuwa fursa ya kuondoa taharuki ya kiusalama katika eneo la Korea ilipotea kutokana jinsi ambavyo Marekani iliamua kuegemea kwenye nia isiyofaa.

Mkutano kati ya viongozi hao ulivunjika baada ya kushindwa kuelewana. Marekani ilieleza kuwa upande wa Korea ulitaka kuondolewa vikwazo vyote vya kiuchumi kama sharti la kuachana na mpango wa silaha za nyuklia, lakini wao hawakuwa tayari kwa hilo.

Aidha, alisema amani ya Rasi ya Korea inategemea kinachofanywa na Ikulu ya Marekani.

Kim amemueleza Rais Putin kuwa hali katika Rasi ya Korea na eneo zima imefikia katika hatua mbaya. Alisema kama hatua hazitachukuliwa kwa wakati huenda itakuwa mbaya zaidi ya taharuki iliyokuwepo awali.

Katika hatua nyingine, Rais Putin alikubali mwaliko wa Kim Jong Un kuitembelea Korea Kaskazini. Imeelezwa kuwa ziara hiyo ifanyika katika muda muafaka utakaoruhusu.

Rais wa Ufaransa ajibu maandamano ya vizibao vya njano
Kimbunga Keneth tayari kimetua Msumbiji