Shirika la Afya duniani (WHO), limesema kuna maambukizi mapya milioni moja ya magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya zinaa kila siku.

Hivyo zaidi ya maambukizi mapya milioni 376 hutokea kila mwaka yakiwemo magonjwa ya Kisonono, kaswende Chlamydia na trichomoniasis.

Shirika hilo la Afya limesema kuwa ukosefu wa mafanikio ya kuzuia kuenea kwa magonjwa ya zinaa ni moja ya sababu za kuenea kwa kasi kiwango cha maambukizi hivyo zinahitajika hatua za dharula za kukabiliana na hali hiyo.

Wataalamu zaidi wanahofu juu ya kuongezeka kwa visa vya magonjwa ya zinaa kuwa kuwa sugu kiasi cha kutotibiwa na dawa zilizopo kwa sasa hii ni kwamujibu wa tathmini iliyofanywa na shirika la Afya duniani juu ya magonjwa manne ya zinaa ambayo yamekuwa yakiripotiwa zaidi maeneo mengi duniani.

Shirika hilo liliangalia utafiti uliochapishwa na kukusanya ripoti kutoka kwa wafanyakazi wake katika nchi mbalimbali zikilinganishwa na tathmini ya mwaka 2012.

Tafiti hizo zimebaini kuwa mtu mmoja kati ya 25 duniani ana walau aina moja ya maradhi ya zinaa, huku baadhi wakiwa na maambukizi ya magonjwa zaidi ya moja kwa wakati mmoja.

Kwa mujibu wa shirika hilo, mwaka 2016 watu wenye miaka 15 hadi 49, milioni 156 walikutwa na trichomoniasis, milioni 127 walikutwa na Chlamydia, milioni 87 walikuwa wagonjwa wapya wa kisonono na milioni 6.3 walikuwa ni wagonjwa wapya wa kaswende.

Ugonjwa wa trichomoniasis husababishwa na maambukizi ya vimelea wakati wa ngono, Chlamydia, kaswende na kisonono huambukizwa kwa bakteria.

Dalili za magonjwa ya zinaa ni pamoja na kutokwa na majimaji yasiyo ya kawaida kwenye uke au uume, maumivu wakati wa kwenda haja ndogo na kuvuja damu kabla ya muda wa hedhi.

Kwa upande wa mwanamke endapo ataambukizwa ugonjwa wa zinaa iwapo ni mjamzito anaweza kujifungua mtoto aliye na ukosefu wa baadhi ya viungo vya mwili au kujifungua mtoto njiti, kipofu, kuwa na matatizo katika viungovyake vya uzazi au matatizo mengine ya kiafya kama kichomi.

 

Wanahabari wapewa mbinu za kukabiliana na Majanga
China na Urusi zatema matumizi ya Dola

Comments

comments