Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema marehemu Dkt. Reginald Mengi alikuwa ni mtu mwenye huruma na moyo wa kusaidia watu mbalimbali na ametumia utajiri wake kuwasaidia Watanzania wengi.

Hivyo kifo chake ni pigo kubwa kwa taifa kwani limepoteza raia makini, mchapakazi na mzalendo.

Kikwete amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kusaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mengi Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

“Nilishtushwa na taarifa za kifo chake, si rahisi kuzungumza kutokana na hali ya majonzi. Nilikuwa Benin katika mkutano wenye ajenda ya kutokomeza malaria ndipo nilipopata taarifa hizi.”

Kikwete amesema marehemu Mengi alikuwa kama kaka yake, kwani walekuwa wakishauriana vitu vingi na kuwasiliana mara kwa mara.

“Hata kabla ya umauti kumkuta nilizungumza na kusalimiana naye kwa sababu alikuwa kama kaka yangu. Nilikubaliana naye kwamba nikirudi safari tutakutana na kuzungumza, kifo chake kimenishtua sana,” amesema.

Kikwete amesema taifa lilitamani kuendelea na Mengi lakini Mungu ameshapitisha uamuzi wake na kilichobaki ni familia kuwa na moyo wa subira.

“Nimezungumza na mtoto wa Mengi aitwaye Abdiel nikamwambia yale aliyoyafanya Mengi yadumishwe na watoto ili bendera ya IPP iendelee kupepea,” amesema Kikwete.

Kikwete amesema ni wakati wa Watanzania kuwaombea watoto na familia ya Mengi ili wayasimamie kwa ufanisi yalioachwa na mpendwa wao.

“Na sisi Watanzania tuwe watulivu tuache uongo wa kutunga mambo badala yake tusubiri watoto wake walioko naye watuambie ukweli.” Amesema

Aidha, Kikwete amewataka watanzania kupuuzia taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijami kuhusiana na sababu za kifo cha Mengi (aliyekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Media), kilichotokea Mei 2 mwaka huu, Dubai, Falme za Kiarabu.

“Kama kweli tunampenda Mengi haya mengine ya uongo uongo, hadithi za kutunga hizi tuachane nazo, tusubiri ukweli, ukweli tutaupata. Alifariki Dubai mdogo wake Benjamin alikuwepo pamoja na binti yake, hao ndio wana ukweli kwahiyo hayo mengine mnayosoma-soma hayo nadhani kwa sasa yaacheni tusibiri wakirudi hao naamini watatuambia ni nini hasa kilitokea na ilikuaje mpaka kile kifo kilitokea,” Dkt. Kikwete aliongeza.

Kuhusu taarifa hizo zinazosambazwa mitandaoni, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro pia amesema anafuatilia yanayoendelea kwenye mitandao kuhusu kifo cha Dkt. Mengi na kwamba wameanza kufanya uchunguzi kwa kufungua ‘dokezo’ ili kubaini ukweli.

Kama alivyosema Dkt. Kikwete, IGP naye aliwataka Watanzania kuwa watulivu na kumpumzisha marehemu na baada ya hapo jeshi hilo litaendelea na uchunguzi wake.

Canelo ampiga Jacobs kutetea ubingwa wa dunia
Video: IGP: Tunafuatilia kifo cha Mengi | Dr Bashiru awashangaa wanaougua Urais CCM