Kitendo cha mchekeshaji, Idris Sultan kuhariri picha ya Rais John Magufuli akijaribu kusherehekea kwa namna yake kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya Mkuu huyo wa nchi kimesababisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumtaka ajisalimishe kituo cha polisi.

Idris aliweka picha hiyo aliyoihariri na kujiweka yeye akionekana amekaa kwenye kiti cha Ikulu, akitania kuwa angependa kubadilishana maisha ya siku moja na mheshimiwa.

Makonda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo ameonesha kutofurahishwa na kitendo cha Idris na ametoa amri ambayo ameiweka pia kwenye Instagram akiambatisha na picha hiyo.

“Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako,” Mkuu huyo wa mkoa ameandika Instagram.

Hata hivyo, dakika chache baadaye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla alitumia mtandao wa Twitter na Instagram kumtetea Idris dhidi ya amri ya RC Makonda, akieleza kuwa atamtafutia wakili wa kumtetea kwakuwa anaamini alichokuwa anakifanya ni utani kama ule wa makabila.

Dkt. Kigwangalla ameandika:

Umoja wa watanzania umejengwa na kuimarishwa sana na ‘utani’ miongoni mwetu. Ndiyo maana tumeweza kuoleana na kufanya kazi kwa kiasi kikubwa bila kugombana ama kubaguana kati yetu. Mfano, kabila kubwa kama la kwetu ama la wasukuma tuna makabila watani zaidi ya 10 hapa nchini. Na ndiyo maana ilikuwa rahisi sana kuuza mgombea wetu mwaka 2015. Mgombea wetu alikuwa anataniana na kuongea/kusalimia kwa lugha za makabila karibu yote nchini ili kujisogeza karibu yao wamuone ‘mwenzetu’. Lakini pia Mhe. Rais wetu anapenda utani, wakati mwingine hutoa utani mbaya kabisa ?, kama hujamzoea unaweza ukatafuta pa kuficha sura yako. Watu wetu wa kila aina jana wamesherehekea birthday yake kwa upendo na Mshikamano wa kipekee.

“Nchi nzima imemuombea dua Rais wetu. Hali iliyoonesha kuwa kweli jana ni siku aliyozaliwa Rais Chuma/Jiwe tunayempenda. Birthday yake ilikuwa ya heshima, ya kiTaifa. Na miongoni mwetu wapo waliotania kuwa wanaenda ikulu kummwagia maji Rais, wengine walimwagia maji picha yake! Ilimradi tu kila mtu alisherehekea birthday ya Mheshimiwa kwa namna yake. Kuna watu wamekuwa wakiiga sauti ya Rais, wakiiga mavazi nk. Sidhani kama ni dhambi, zaidi kwa mwanamkakati kama mimi, nikifanya tathmini yangu, mara moja naona kuwa Rais anapendwa na watu wake. Watu wanaona Rais ni mali yao. Wanajihusisha naye.

“Na hii ni dalili kuwa mwakani Rais atapita kwa upepo wa kisulisuli, pengine zaidi ya asilimia 90! My take: tuwaache watu wetu wamsherehekee Rais wao, huyu ni mtu wao, ni mali yao! Tusimtenge na watu wake. Imagine Rais angekuwa haleti utani hata kidogo, uso wa mbuzi mwanzo hadi mwisho, na sisi tukauona upande wake wa pili kwamba ni ‘binadamu’ mwenye utu, upendo na huruma, unadhani tungekuwa tunanyoosha mikono kumshauri kwa dhati kabisa kwenye vikao?! Kwanza tungezikimbia teuzi! ???. Nani angebaki kumsaidia kazi hii ngumu aliyonayo? Utani wa Rais unalainisha vyuma kidogo. Tuwaache watanzania wamfurahie Rais wao jamani!

Sheria ya mfumo wa nidhamu kazini yapikwa
Zahera aendelea kupambana na hali yake