Wakati shule za msingi na sekondari zikifunguliwa leo baada ya kufungwa kutokana na tadhari ya virusi vya corona, mitihani ya kidato cha sita na ualimu inaanza leo na inatarajiwa kumalizika Julai 15.

Katibu Mtendaji wa Baraza ka Mitihani la Tanzania, Dkt. Charles Msonde amesema tayari maandalizi yote kwaajili ya mitihani yamekamilika ikiwepo kusambazwa kwa mitihani, vitabu vya kujibia na nyaraka nyingine muhimu, Tanzania bara na visiwani.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema mitihani ya kidato cha sita ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kwa kupima maarifa, stadi na umahiri wa wanafunzi katika yale yote waliyojifunza kwa miaka miwili.

Amebainisha kuwa matokeo ya mitihani huo hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu na vyuo vya kati katika fani mbalimbali za utaalamu wa kazi.

Amesema mtihani huo utafanyika katika jumla ya shule za sekondari 763, vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 239 na vyuo vya ualimu 85 Tanzania bara na Zanzibar.

Katika mtihani wa kidato cha sita jumla ya watahiniwa 85,546 wamesajiliwa kufanya mtihani huo ambao kati yao watahiniwa wa shule ni 74,805 na watahiniwa wa kujitegemea ni 10,741.

“Aidha watahiniwa wanye vipaji maalumu wapo 113, kati ya hao 72 ni wenye uoni hafifu, 19 wasioona, 19 wenye ulemavu wa kusikia na watatu wenye ulemavu wa akili” ameeleza Dkt. Msomde.

Amesisitiza kuwa, baraza la mitihani halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kujihususha au kusababisha udanganyifu wa mitihani, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu na kanuni za utumishi wa umma.

Waziri Kalemani Atoa Siku 7 wananchi Mwanza kuwekewa Umeme
DAS Kisarawe atenguliwa kwa kashfa ya kuchukua wake za watu