Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amewaagiza viongozi wa Manispaa kupanga tarehe za kukutana na wananchi walimuonesha mabango ya kero mbalimbali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa kwenye ziara ya kikazi mkoani humo Oktoba 4, mwaka huu.

Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo mjini Singida baada ya wananchi kugomea kero zao kusikilizwa na viongozi wa idara za Serikali ambao wanawatuhumu kushindwa kuzitatua hapo awali hali iliyopelekea kufikisha ujumbe kwa njia ya mabango kwa Waziri Mkuu.

Wengi wa wananchi hao wanalalamikia migogoro ya ardhi ikiwemo madai ya fidia ya viwanja namba 23 na eneo lililoko nyuma ya mtaa wa Ginnery na kupinga rufaa ya kesi ya ardhi iliyotolewa hukumu na baraza la ardhi la wilaya ya Singida.

Madai mengine ni kiwanda cha mafuta ya alizeti kumilikiwa na wajanja wachache, kutokamilika kwa mradi wa ujenzi wa matundu ya vyoo na mabweni shule ya msingi Mtinko tangu mwaka 2017 na mkopo wa Saccos fedha kutoka NSSF milioni 160 zilizokuwa wakopeshwe wanachama badala yake kupelekwa kwa vigogo Singida mjini.

Hata hivyo kati ya migogoro 27 iliyowasilishwa kwa Waziri Mkuu kwa njia ya mabango zaidi ya 20 kati ya hiyo inahusu masuala ya ardhi upande wa fidia baada ya maeneo ya wahusika kudaiwa kuchukuliwa na serikali kwa matumizi mengine.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya kuyaona na kupokea mabango hayo alimuagiza Mkuu wa Mkoa kutatua changamoto za wananchi hao ambapo jana Oktoba 28, 2019 alikutana nao akiwa na viongozi wa idara za serikali kwa ajili ya kuwasikiliza na kutafuta njia ya kuzitatua kwa pamoja.

Serikali yakemea ubadhirifu wa dawa
TMA yawataka wakulima kutumia vyema mvua za masika