Pichani: Keisha akiwa na Rais mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete (Maktaba)

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM), Khadija Shabani Taya maarufu kama Keisha, amewajibu wanaokosoa hatua ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Bashiru Ally kumuombea msamaha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwenye ibada ya kumuaga Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dkt. Reginald Mengi.

Dkt. Bashiru alitumia dadika chache za neno lake kwenye ibada hiyo kumuombea msamaha Makonda kwa kauli aliyoitoa iliyotafsiriwa na wengi kuwa ilijenga taswira ya kubeza kabila fulani.

Kupitia mtandao wa Instagram, Keisha amejibu ujumbe wa William Malecela maarufu kama Lemutuz aliyekosoa vikali hatua hiyo ya Dkt. Bashiru, ambapo mjumbe huyo wa Kamati Kuu ameeleza kuwa suala alilolifanya ni la kiungwana zaidi.

“Sitaki kuamini ninachokiona lemutuz hapo Katibu Mkuu amekosea wapi na kwanini umshtumu kiongozi wako wa chama kwenye mitandao na si kwenye vikao kama kweli umeona kosa. Hivi unataka kuniambia kumuombea mtu msamaha kwa mtu aliyehisi amekosewa si sawa? Mi nadhani Katibu hajakosea kwa sababu msamaha huombwa mtu aliyekwazika kwa jambo hata kama RC hakukosea ila watu wamekwazika na kauli tu ambayo haikuwa na lengo baya zaidi ya utani ila sasa wewe ndo umeharibu zaidi kwa kuendeshwa na hisia za urafiki na kufikia kumkosea heshima Katibu Mkuu ambaye ndiye mtendaji mkuu wa chama na wewe ukiwa ni mwanachama; na sijategemea mtu kama wewe kufanya kosa kama hilo @lemutuzi_superbrand SHAME ON YOU,” ameandika Keisha.

Katika ibada hiyo, Dkt. Bashiru alimuombea msamaha Makonda baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kueleza kukwazika na kauli ya Makonda kwa niaba ya wengi aliosema anawawakilisha.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu DkFredrick Shoo alimpa nafasi Makonda kuzungumza ambapo alishukuru kwa hatua ya Katibu Mkuu kumuombea msamaha pamoja na Mbowe kuweka wazi alivyokwazika.

Makonda alieleza kuwa hakuwa na nia mbaya kupitia kauli yake lakini alitafsiriwa tofauti. Hivyo, aliomba radhi kwa tafsiri ya alichokizungumza.

Chanzo cha mzozo huo ni kauli ya Mkuu huyo wa Mkoa kutoa kauli iliyoeleza kuwa ni vigumu kumuona chaga anatoa pesa yake kuwasaidia watu wenye mahitaji kama walemavu na kwamba Dkt. Mengi alikuwa wa aina yake.

 

Busega sasa kuondokana na tatizo la Maji
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Mei 11, 2019

Comments

comments