Syria imelaani kauli aliyoitoa Rais wa Marekani, Donald Trump kwamba sasa ni wakati wa kuitambua milima ya Golan kuwa ni sehemu ya Israel na kuapa kwamba italirejesha eneo hilo kwenye umiliki wake kwa njia yeyote ile.

Shirika la habari la Syria limenukuu chanzo kutoka wizara ya mambo ya nje na kusema kuwa Rais Donald Trump ameonesha upendeleo wa Marekani kwa Israel na kwamba hatua hiyo haiwezi kubadili ukweli, na eneo hilo litabaki kuwa la Syria.

Kwa upande wake Iran imesema kuwa kauli ya Trump haikubaliki na siyo halali huku Urusi ikieleza kwamba kubadili hali ya eneo la Golan ni kuvunja maazimio ya umoja wa mataifa.

Naye Rais wa Uturuki, Reccep Tayip Erdogan amelaani vikali pia tamko hilo la Trump na kusema kuwa hatarajii Uturuki na Jumuiya ya nchi za kiislamu zikakaa kimya ama kunyamazia suala hilo nyeti.

Aidha, Iran na Urusi ina vikosi nchini Syria vinavyo muunga mkono Rais Bashar Al Assad katika vita vinavyoendelea nchini humo huku Iran ikipeleka vikosi vyake yenyewe na kupeleka wanamgambo wa kishia inaowasaidia kama vile Hezbollah.

Hata hivyo, siku ya alhamisi Rais Donald Trump aliandika katika mtandao wa Twitter kwamba baada ya miaka 52, ni wakati muafaka kwa Marekani kutambua udhibiti wa Israel katika milima ya Golan, akiliita eneo hilo kuwa la kimkakati na kiusalama kwa Taifa la Israeli na uthabiti wa kanda nzima.

 

 

Wanafunzi wa vyuo vikuu mikononi mwa Uhamiaji
TBS yawataka wazalishaji kuchangamkia fursa