Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Njombe mkoani humo, Antoni Katani akiambatana na baadhi ya viongozi wa chama hicho wilayani wamezitembelea familia mbili tofauti ambazo hivi karibuni zimepoteza watoto kwa kuuawa na watu wanaodaiwa kujihusisha na imani za kishirikina.

Familia zilizotembelewa na viongozi hao ni familia ya Gorden Mfugale pamoja na familia ya Rabia Mlelwa wote wakazi wa Kata ya Mjimwema mjini Njombe ambao watoto wao waliuawa ambapo mtoto wa Rabia Mlwelwa alifariki dunia baada ya kukatwa koromeo.

Akizungumza kwa nyakati tofauti akiwa nyumbani kwa wafiwa eneo la Mjimwema mjini Njombe, Katani amesema kuwa licha ya sakata hilo kutulia kutokana na Serikali kuimarisha ulinzi katika pembe zote za mkoa huo bado chama cha mapinduzi CCM kinaendelea kutoa pole na kuwafariji wafiwa ambao wamepoteza familia zao bila hatia.

‘’Poleni sana wafiwa wote tunaamini haya ni mapenzi ya mwenyezi mungu hatuna budi kuyapokea lakini vifo vya watoto wetu vimesababishwa na watu wachache wasio wema, mwenyekiti wetu wa chama ngazi ya taifa ameendelea kututuma sisi wasaidizi wake kuja kutoa pole,’’amesema Katani

Kwa upande wao wanafamilia waliopoteza watoto wao wameushukuru uongozi wa chama cha mapinduzi CCM ngazi ya wilaya na mkoa wa Njombe pamoja na Taifa kwa ujumla kwa kuendelea kuwafariji katika kipindi kigumu wanachopitia.

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 23, 2019
Simba yaendelea kutakata, yailamba Azam FC 3-1