Rapa kutoka Atlanta Marekani, Kanye West leo amekutana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni katika Ikulu ya nchi hiyo.

Kanye West ambaye yuko nchini humo na mkewe Kim Kardashian pamoja na mtoto wao North West, anatarajia kurekodi albam yake mpya akiwa ndani ya nchi hiyo.

Katika mkutano huo, Kanye ambaye hivi karibuni amejibatiza jina jipya la ‘Ye’, alimpa Rais Museveni zawadi ya raba nyeupe (sneakers).

Rais Museveni alisema kuwa wamefanya mazungumzo yenye matunda, kikubwa ikiwa ni kuhusu kutangaza vivutio vya utalii pamoja na sanaa.

Kanye na familia yake wanaendelea na ziara yao wakitembelea pia mbuga za wanyama  na inadaiwa kuwa sehemu ya nyimbo zake zitarekodiwa katika mbuga hizo.

Uganda imeutumia vizuri ugeni wa Kanye West katika kuhakikisha inatangaza kwa nguvu vivutio vya utalii duniani, hasa kupitia mitandao ya kijamii.

Moja kati ya picha zilizosambazwa na raia wa Uganda mitandaoni ni picha inayomuonesha akiwa amejitanda mwilini bendera ya nchi hiyo akiwa na kikuza sauti (microphone).

Rapa huyo ambaye pia ni mtayarishaji wa nyimbo kabla ya kwenda Uganda alikutana na Rais wa Marekani Donald Trump.

Somalia yaadhimisha siku ya 'Black Day'
Prince Harry, Meghan waanza ziara ya kikazi Australia