Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) limesema kuwa matokeo ya uchaguzi wa Rais yaliyotangazwa na Tume Huru ya Taifa Uchaguzi ya nchi hiyo (CENI) hayaakisi taarifa zilizokusanywa na waangalizi wake.

Jana alfajiri, CENI ilitangaza matokeo ya uchaguzi ya urais ambayo yalimtangaza Felix Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia 38.5, akiwazidi Emmanuel Shadary wa chama tawala na Martin Fayulu aliyekuwa anaungwa mkono na vyama kadhaa vya upinzani.

Rais Mteule wa DRC, Felix Tshisekedi

“Tunaona matokeo ya urais yaliyotangazwa na CENI kuwa hayaendani na takwimu zilizokusanywa na waangalizi wetu katika vituo vyote vya kupigia kura nchini,” amesema Padri Donatien Nshole ambaye ni msemaji wa Baraza la Maaskofu nchini humo.

Wiki iliyopita, Kanisa hilo lilisambaza waangalizi 40,000 kwenye vituo vya kupigia kura nchini humo. Baada ya kukusanya takwimu zake, ilieleza kuwa inafahamu mshindi wa uchaguzi huo lakini ikaitaka CENI kuhakikisha inamtangaza mshindi kwa haki.

Mwanadiplomasia Mwandamizi wa Ufaransa, Nshole alieleza jana kuwa takwimu za Kanisa Katoliki zimeonesha kuwa Martin Fayulu ndiye aliyeshinda uchaguzi huo na sio Tshisekedi.

Takwimu za CENI zinaonesha kuwa Tshisekedi alipata kura Milioni 7 na Fayulu akimfuatia kwa kura Milioni 6.4 huku mgombea wa chama tawala, Emmanuel Shadary akiambulia kura Milioni 4.4.

Tshisekedi anatarajiwa kuapishwa Januari 25 mwaka huu kuwa Rais wa Tano wa DRC akihitimisha utawala wa miaka 18 wa Rais Joseph Kabila. Anaandika historia mpya ya kuwa rais wa kwanza aliyekabidhiwa madaraka kwa njia ya kidemokrasia kupitia sanduku la kura.

R Kelly apanga kukimbilia Afrika, wanaodai aliwabaka wacharuka
Ki-Jana aishangaza Liverpool kwa kumdhibiti vikali Mo Salah