Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amesema kuwa Kambi za Kitaaluma mkoani Simiyu kwa wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha Sita, ambayo ni madarasa yanayofanya Mitihani ya Taifa ya kuhitimu elimu ya Msingi na Sekondari zitakuwa endelevu.

Ameyasema mkoani humo wakati akihitimisha Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha sita iliyofanyika kwa takribani mwezi mmoja katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, ikihusisha wanafunzi 1166 kutoka katika shule 12 mkoani humo.

Amesema kuwa Mkoa huo utaendelea kufanya jitihada na kuboresha zaidi kambi hizo huku akieleza kuwa ameshawaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani humo kutenga fedha kwa ajili ya motisha kwa walimu na wanafunzi watakaokuwa wakifanya vizuri.

“Kambi za kitaaluma zitaendelea kuwepo katika kipindi chote nitakacho kuwepo na tutaendelea kuboresha, mwaka huu nimewaambia Wakurugenzi ni lazima kila Halmashauri itenge fedha kwa ajili ya motisha katika elimu, motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri,” amesema Mtaka.

Katika hatua nyingine Mtaka amewashukuru walimu, wanafunzi na wadau mbalimbali waliochangia kufanikisha kambi ya kidato cha sita, huku akiwasisitiza wanafunzi hao kuendeleza juhudi walizozionyesha wakiwa kambini na kutumia mbinu walizopewa na walimu mahiri ili waweze kufanya vizuri mitihani yao ya mwisho.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato kutoka Jijini Mwanza, Nicodemo Ntabindi amewaonya wanafunzi wa Kidato cha sita kutojihusisha na masuala ya mapenzi badala yake wajikite katika masomo tu kwa sasa ili waweze kufikia ndoto zao.

Kwa upande wao wanafunzi waliokuwepo katika kambi hiyo ya Kitaaluma wamesema kambi hiyo imekuwa msaada kwa wanafunzi kwa kuwa imechangia kuwasaidia kupata ufumbuzi wa mada ngumu zilizokuwa zinawapa shida na kuahidi kufanya vizuri katika mtihani wa Taifa kutokana na namna walivyoandaliwa vema.

 

 

Video: Tanasha ameachia ngoma mpya, Mama Diamond ampa tano, Diamond aufyata
Sir Lanka yapiga marufuku mavazi ya Nikabu kwa wanawake