Kamati imesikiliza malalamiko ya timu ya Dodoma FC dhidi ya JKT Oljoro katika mechi yao iliyochezwa Januari 21, 2018 kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi. Malalamiko hayo yalikuwa na sehemu mbili; moja ni uhalali wa mchezaji wa JKT Oljoro, Haki Rubea kuwa hakuwa na leseni, na mbili ni kudai kuwa Mwamuzi na Mwamuzi Msaidizi Namba Moja walikataa bao lao halali.
Baada ya kupitia malalamiko hayo, Kamati imebaini kuwa Haki Rubea ni mchezaji wa JKT Oljoro mwenye leseni namba 961111011 iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), hivyo ni mchezaji halali (qualified player). Vilevile Kamati haina mamlaka ya kukubali bao ambalo limekataliwa na Mwamuzi uwanjani. Hivyo, Kamati imetupa malalamiko ya Dodoma FC kwa hoja zote mbili.
Hata hivyo, Kamati imejiridhisha kuwa Kamishna wa mechi hiyo Paul Opiyo na Mwamuzi wa Akiba, Gilbyrth Mrina walifanya makosa kumruhusu mchezaji huyo kucheza bila kuonyesha leseni yake, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(16) na 14(17) za Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Kamati imeteua wajumbe watatu kupitia mkanda wa mechi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine itachunguza kiwango cha uchezeshaji cha Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Emmanuel Muga na Mwamuzi wa Akiba, Gilbyrth Mrina na kuwasilisha taarifa yake kwa ajili ya hatua Zaidi.

BFT: Si kweli timu ya taifa inaishi kwa chai na chapati
Maamuzi kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi – Ligi daraja la kwanza