Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amehojiwa leo na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kufuatia kauli yake aliyoitoa bungeni, akiunga mkono kile ambacho kilisababisha mbunge mwenzake Halima Mdee kusimamishwa kushiriki vikao vya Bunge.

Kamati hiyo imemhoji Lema mara tatu kwa jumla ya dakika 132 kwa muda tofauti, kuanzia asubuhi hadi saa kumi na moja na dakika 58 jioni.

Hatua ya kuhojiwa ilitokana na maelekezo ya Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson kwa kamati hiyo, baada ya Lema kueleza kuwa anaunga mkono kauli ya Mdee pamoja na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, Profesa Mussa Assad kuwa ‘Bunge ni dhaifu’.

Kamati hiyo inatarajia kutoa ripoti yake bungeni kesho ambapo hatma ya sakata hilo kwa Lema itajulikana. Je, itakuwa kama ilivyomkuta Mdee au atachukuliwa tofauti? Kesho yote yatafahamika.

Naibu Spika aliagiza Kamati kuhakikisha wanakamilisha kumhoji Lema leo ili kesho wawasilishe ripoti ya mahojiano hayo bungeni kwa ajili ya hatua zaidi.

Sakata hilo lilianza baada ya CAG kutoa kauli akidai kuwa ‘Bunge ni dhaifu’, alipokuwa akizungumza na kituo cha redio cha kimataifa akiwa Marekani.

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Aprili 4, 2019
Papa Francis: Messi sio Mungu

Comments

comments