Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ametoa tahadhari kwa watu ambao wamejipanga kufanya vurugu katika uchaguzi wa marudio wa jimbo la Kinondoni uliopangwa kufanyika hapo kesho.

Ameyasema hayo hii leo jijini Dar es salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa kuna kundi la watu wachache kutoka katika chama kimoja cha siasa ambao wamepanga kufanya vurugu kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kesho (Jumamosi) katika Jimbo la Kinondoni.

“Jeshi la Polisi limejipanga vizuri zaidi ya uchaguzi uliopita 2015, tulikuwa na majimbo kadhaa ndani ya Dar es Salaam lakini kwa huu wa marudio tuna jimbo moja tu hili la Kinondoni na kwa sababu hiyo ni seme kwamba Jeshi la Polisi tumejipanga imara na kuhakikisha hakuna mtu atakayeruhusiwa kuingia na kufanya vurugu kwenye uchaguzi,”amesema Kamanda Mambosasa

Hata hivyo, Kamanda Mambosasa amesema kuwa ni vyema kwa mtu yeyote ambaye ameshawishiwa kufanya vurugu katika zoezi la kupiga kura ni bora akajitoa mwenyewe kuliko kuingia katika matatizo makubwa kwa sababu hakuna atakayeachwa akafanya fujo kisha akaendelea kupiga hatua mbele.

 

Raia wa Urusi washitakiwa kwa kuchakachua ushindi wa Trump
Dkt. Nchemba: Demokrasia si kukatana mapanga