Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe amewataka waumini wa kanisa lake kuwa imara kama yeye, kwani hayumbishwi kwa upepo kama nyasi.

Askofu Kakobe ameyasema hayo jana alipokuwa anaongoza ibada kanisani kwake jijini Dar es Salaam. Amesema amepitia mengi na hakuwahi kuyumba kwa namna yoyote.

Amesema kuwa hata kama atapitishwa kwenye mambo magumu mfano wa kupita kwenye moto, yeye na kanisa lake watashinda na kung’aa kama dhahabu.

“Hata wafanye nini, mimi siyo nyasi zinazotikiswa na upepo. Katika hayo yote nitashinda zaidi ya ushindi,” alisema Askofu Kakobe.

“Kanisa langu sio la kuombea watu na kuwaponya magonjwa. Hili ni kanisa ambalo hata likipita kwenye magumu kama Lazaro na Ayubu, halitatikisika,” anakaririwa.

Aliwataka waumini wake kuhakikisha wanapopita katika magumu wakumbuke kuwa Shetani huwaogopa wacha Mungu na hufanya jitihada za kuwaangusha, hivyo wanapaswa kusimama na kuvumilia kama Ayubu.

Aidha, Askofu Kakobe anatakiwa kufika katika ofisi za Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano. Bado kiini cha mahojiano hayo hakijafahamika.

Hivi karibuni, Mhubiri huyo alichunguzwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu kumbukumbu za kulipa kodi na ripoti yake iliwekwa hadharani.

Ukaguzi huo ulikuja baada ya kauli ya Askofu huyo kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali. Hata hivyo, ilibainika kuwa hana akaunti katika benki yoyote nchini.

‘Miss Tanzania Mpya’ yasukwa, Basila aipaka rangi
JPM aahidi kutowaangusha viongozi wa dini