Leo Mei 8, 2017 maelfu ya watu wamejitokeza kuhudhuria ibada ya pamoja kuwaaga wanafunzi zaidi ya 30 wa shule ya msingi ya Lucky Vicent waliofariki katika ajali ya barabarani baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutumbukia kwenye korongo la mto Mrera Wilayani Karatu, Arusha.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameendelea kuelezea jinsi alivyopatwa na huzuni kutokana na ajali hiyo.

Kupitia ukurasa wake wa Tweeter Rais Magufuli ameandika kuwa “Nimepatwa na uchungu na majonzi makubwa ninapoyaona majeneza ya watoto na walezi wao waliopoteza maisha katika ajali ya basi huko Arusha.

Tumewapoteza mashujaa wetu katika elimu,” amesema.

Rais Magufuli alituma salamu za rambirambi Jumamosi ambapo alisema kuwa ajali hiyo imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia taifa na imesababisha uchungu, huzuni na masikitiko makubwa kwa familia za marehemu na Taifa kwa ujumla.

“Muhimu kwa sasa tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema, majeruhi wapone haraka na wote walioguswa na msiba huu wawe na moyo wa subira, ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.”

Akiongoza waombolezaji, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amevitaka vyombo husika vihakikishe suala la usalama barabarani linapewa kipaumbele.

“Nawaasa madereva kuwa makini wawapo barabarani na serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara,” amesema.

Katika maombolezo hayo, pia Waziri wa elimu wa Kenya Dkt Fred Matiang’i ni mmoja wa wageni kutoka nje ya Tanzania waliohudhuria ibada hiyo, amewapa pole Watanzania kwa msiba huo.

Amesema kuwa Kenya itaendelea kuwa pamoja nasi kwenye kipindi hiki kizito cha msiba huu mzito. Amesema msiba huu si wa Tanzania peke yake ni wa wote hata Kenya Rais Kenyatta na mkewe wametoa pole sana na kuwaombea.

“Kenya itaendelea kuwa pamoja nanyi kwenye kipindi hiki kizito cha msiba huu mzito uliowafika. Msiba huu si wa Tanzania peke yake ni wa wote hata kwetu Kenya Rais Kenyatta na mkewe wanawapa pole sana na kuwaombea,” amesema.

Wanafunzi hao wa darasa la saba walifariki dunia pamoja na walimu 2 na dereva wa gari la shule hiyo ya msingi ya Arusha baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika eneo Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.

Wanafunzi na walimu hao walikuwa wakitoka shuleni kwao kwenda shule ya msingi iitwayo Tumaini kwa ajili ya kufanya mtihani wa ujirani mwema na walipofika katika eneo la Rhotia Marera basi walilopanda liliacha njia na kisha kutumbukia korongoni. Wanafunzi watatu walijeruhiwa.

 

"Lionel Messi" nusura aswekwe mahabusu
Wabunge wafanya tendo jema, waachia posho zao kuwafariji wafiwa