Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameeleza kile kinachoweza kuwa moja kati ya sababu za kufikia uamuzi wa kumuondoa kwenye baraza la mawaziri, January Makamba, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Akizungumza leo Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwaapisha George Simbachawene ambaye anachukua nafasi ya Makamba na Hussein Bashe aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Mifugo, Rais Magufuli aligusia jinsi ambavyo hakufurahishwa na utekelezaji wa agizo la kusitishwa kwa matumizi ya mifuko ya plastiki.

Alisema kuwa ilichukua takribani miaka minne kutekeleza agizo hilo ingawa lilitolewa mara kadhaa na Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu, hadi yeye mwenyewe alipoamua kutoa amri.

“Nakumbuka suala la mifuko ya plastiki lilichukua muda mrefu, takribani miaka minne. Nikasaini, haikutekelezwa. Makamu wa Rais akazungumza weee.., haikutekelezwa. Waziri Mkuu akazungumza Bungeni, haikutekelezwa. Mpaka mwishoni hapa nilipotoa amri ndipo likaanza kutekelezwa,” alisema Rais Magufuli.

Rais alimtaka Simbachawene kuwa tofauti na kutekeleza kwa vitendo kiapo chake akijifunza kutoka kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Rais Magufuli aligusia kutoridhishwa na ucheleweshwaji wa vibali vinavyotolewa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), akimtaka Waziri Simbachawene kuhakikisha anahuisha utolewaji wa vibali kwa wawekezaji kwa haraka.

Naye Simbachawene alipokuwa akitoa neno la shukurani, alieleza kuwa kwa kuzingatia uzoefu wake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, amekuwa akiona fedha nyingi zinatolewa kwa ajili ya miradi ya mazingira lakini utekelezaji wa miradi hiyo hauridhishi.

“Nimeona numbers (tarakimu) lakini kinachokwenda kwenye mazingira kama mazingira hukioni… na hasa tunavyoona hali ya uharibifu wa mazingira kwenye maeneo tunayoishi,” alisema.

“Vyanzo vya maji vinazidi kutoweka, misitu inatoweka, misitu inakauka, mito inakauka, mabwawa yanakauka lakini fedha zinazotajwa kuingia kwenye nchi ni nyingi lakini hazitatui matatizo na yanaendelea,” alisema Simbachawene.

Aliahidi kuwa atashirikiana na wataalam wa Wizara yake kutatua changamoto za mazingira na kuleta mabadiliko chanya.

Rais Magufuli ampa Bashe mtihani, amkumbusha ‘machachali’ ya bungeni
Kenya: Mlinzi wa Spika auawa kwa Risasi

Comments

comments