Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema kuwa Uhuru uliopatikana Desemba 9, 1961 ni mwanzo wa kutafuta Uhuru wa kiuchumi ambao ameutaja kuwa ndio mgumu zaidi kupatikana.

Ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es salaam wakati akitoa salamu za Kumbukumbu ya miaka 57 ya Uhuru ikiwa taifa linaelekea kwenye maadhimisho ya siku hiyo hapo Desemba 9.

Amesema kuwa katika kuadhimisha miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, ameagiza fedha zilizokuwa zitumike kuadhimisha siku hiyo, zikajenge hospitali itakayoitwa ‘Uhuru hospital’ jijini Dodoma.

“Watu wengi wameshahamia Dodoma, hii imefanya mahitaji ya huduma za kijamii ikiwemo Afya jijini humo kuongezeka, hivyo tumeamua kujenga hospitali nyingine kubwa itakayosaidiana na hospitali ya Mkapa iliyopo UDOM na hospitali ya Mkoa wa Dodoma,”amesema JPM

Aidha Kwa mujibu wa Ibara ya 45 Ibara ndogo ya kwanza Rais Magufuli ametangaza kuwasamehe Wafungwa 4,477. Wafungwa 1,076 watatoka siku ya Maadhimisho ya Uhuru yani Desember 9, 2018, msamaha huo utawahusu Wafungwa Wagonjwa, Wazee kuanzia miaka sabini na zaidi, Wafungwa wakike walioingia Gerezani wakiwa Wajawazito.

Hata hivyo, Rais Magufuli ameongeza kuwa ambao hawatohusika na msamaha huo ni wale ambao wanaotumikia baadhi ya adhabu zikiwemo Kunyongwa, Kifungo cha maisha, biashara ya Dawa za kulevya, biashara za binadamu, kukutwa na viungo vya Binadamu, Walionajisi na waliowapa mimba Wanafunzi.

 

 

Lugola amkalia kooni Afisa Elimu, amtaka atoe maelezo ya kutosha
Ni kesho: Je, umeshampigia kura Queen Elizabeth kuwa Miss World 2018?