Bingwa wa dunia wa masumbwi wa uzito wa juu, Anthony Joshua amesema yuko tayari kupambana na bingwa mwenzake ambaye hajawahi kupoteza pambano, Deontay Wilder ili kumpata bingwa wa kiwango cha juu zaidi yaani ‘undisputed.

Joshua ambaye alitegemewa kupambana na Alexander Povetkin baada ya kumshinda kwa pointi Joseph Parker, amesema kuwa anataka kukata mzizi wa fitna kati yake na mbabe huyo na kwamba tayari wameshaitumia timu ya Wilder ofa ya pambano.

Kwa mujibu wa promota wa Joshua ambaye anaandaa pambano hilo nchini Uingereza, wameitumia timu ya Wilder ofa ya $ 12.5 milioni lakini timu hiyo imeikataa.

Timu ya Wilder imetaka kuwe na mgawanyo wa asilimia 60-40, wakidai kuwa pambano hilo linaweza kuingiza zaidi ya $100 milioni, hivyo wanataka $40 milioni.

Hata hivyo, Joshua amedai kuwa kama Wilder anaamini watingiza kiasi hicho cha fedha basi wao wampe $50 milioni ambayo ni sawa na mgao wa pasu kwa pasu.

“Wanipe mimi $50 milioni kabla ya pambano, mimi nitasaini mkataba wa pambano kesho tu. Wasiishie kuzungumzia kwenye mitandao ya kijamii, warudi mezani wajibu kwa barua pepe kama watu weledi,” alisema AJ.

AJ amesisitiza kuwa pambano hilo ni lazima lifanyike kwa maslahi ya historia ya masumbwi ya uzito wa juu katika kizazi hiki.

Bingwa wa pambano kati yao ataweka rekodi ambayo haijawahi kufikiwa, ya kuwa bingwa wa mikanda yote minne mikubwa kwa wakati mmoja.

Video: JPM awapandisha vyeo wanajeshi
Spika abadiri utaratibu wa kuingia Bungeni