Shirikisho la soka nchini Nigeria (NFF) limethibitisha uteuzi wa aliyewahi kuwa nahodha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Joseph Yobo, kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya wakubwa (Super Eagles).

Yobo mwenye umri wa miaka 39, atafanya kazi ya kumsaidia kocha kutoka nchini Ujerumani Gernot Rohr, huku akichukua nafasi ya Imama Amapakabo.

Mtihani wa kwanza kwa mkongwe huyo unatarajiwa kuwa kwenye mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika dhidi ya Sierra Leone Machi 23, na kicha mchezo wa pili dhidi ya taifa hilo la Afrika magharibi Machi 31.

Nigeria inaongoza msimamo wa kundi L ikifikisha alama sita, baada ya kucheza michezo miwili, ikifuatiwa na Benin yenye alama tatu, Lesotho ipo nafasi ya tatu kwa kumiliki alama moja sawa na Sierra Leone.

Beki huyo wa zamani wa klabu za Everton, Norwich City (England) na Fenerbahce (Uturuki), anaendelea kukumbukwa na mashabiki wengi wa soka duniani kwa kuwa mchezaji anaeshika namba mbili kwa kushiriki michezo mingi ya timu ya taifa ya Nigeria (Super Eagles).

Mchezo wake wa kwanza kwa timu ya taifa ya wakubwa alicheza dhidi ya Zambia mjini Chingola mwaka 2001, na alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2013 Afrika kusini.

Alifanikiwa kucheza fainali sita za mataifa ya Afrika kuanzia mwaka 2002 hadi 2013, huku akicheza fainali tatu za kombe la dunaini mwaka 2002, 2010 na 2014, kwa kushiriki michezo kumi.

Yobo aliweka historia ya kuwa muafrika wa kwanza kuwa nahodha wa kikosi cha klabu ya Everton Oktoba 2007, na aliitumikia klabu hiyo katika michezo zaidi ya 250, huku akiisaidia kushiriki ligi ya mabingwa barani Ulaya mwaka 2005.

Pia alikua sehemu ya kikosi cha Everton kilichoshindwa kutwaa ubingwa wa kombe la FA mwaka 2009, baada ya kufungwa na Chelsea kwenye mchezo wa fainali.

Neymar hatarini kuikosa Borussia Dortmund
Kocha wa Misri asubiri maamuzi ya Mohamed Salah

Comments

comments