Meneja wa Man Utd, Jose Mourinho ameutahadharisha uongozi wa klabu hiyo kufanya usajili kabla ya dirisha la usajili wa majira ya kiangazi halijafungwa juma hili, ili kuepuka kufanya vibaya msimu ujao wa ligi ya England.

Mourinho ametoa tahadhari hiyo mara baada ya mchezo wa mwisho wa kujipima nguvu katika kipindi hiki cha maandalizi ya msimu mpya wa ligi dhidi ya mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, walioibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri.

Mourinho amesema suala la kufanya usajili kwenye kikosi chake kabla ya kumalizika kwa muda wa dirisha la usajili haliepukiki na kama halitofanyiwa kazi kuna hatari ya kufanya vibaya msimu ujao.

Amesema mpaka sasa hajaridhishwa na mwenendo wa kikosi chake tangu walipoanza kujiandaa na msimu mpya wa ligi na mara kadhaa ametoa tahadhari hiyo kwa viongozi.

“Mtendaji wangu mkuu anafahamu nini ninachokihitaji, bado tuna siku chache kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, tusubiri ili tuone kama mambo yatakaa sawa,” alisema Mourinho alipohojiwa na televisheni ya Man Utd (MUTV).

“Wapinzani waliopambana nasi tangu tulipoanza kujiandaa na msimu mpya, wote wamejidhatiti vizuri na wameonesha kuwa katika mustakaali mzuri wa kufanya vizuri msimu ujao lakini kwa kikosi changu imekuwa tofauti na kila shabiki duniani anaona udhaifu wetu,” aliongeza.

Tayari Man utd wameshatumia zaidi ya Pauni milioni 80 katika kipindi hiki cha dirisha la usajili wa majiranya kiangazi, baada ya kumsajili kiungo wa kibrazil kutoka klabu ya Shakhtar Donetsk Fred pamoja na beki wa pembeni Diogo Dalot akitokea FC Porto.

Hata hivyo uongozi wa Man Utd umeonyesha kusita kufanya usajili wa pesa nyingi katika kipindi hiki, baada ya kufanya hivyo misimu miwili iliyopita kwa kumsajili Paul Pogba kwa Pauni milioni 89 na Romelu Lukaku kwa Pauni milioni 75.

Wachezaji waliopendekezwa na Mourinho ili wasajiliwe kabla ya dirisha la usajili kufungwa ni Harry Maguire (Leicester City), Ivan Perisic (Inter Milan), Jerome Boateng (Bayern), Toby Alderweireld (Tottenham), Yerry Mina (Barcelona) na Willian (Chelsea).

Man Utd watafungua msimu mpya wa ligi siku ya ijumaa kwa kucheza na mabingwa wa England msimu wa 2015/16 Leicester City, kwenye uwanja wa Old Trafford.

Video: Waziri Kigwangalla asimulia alivyonusurika, Uvumilivu wa Lissu umefika mwisho
Si kila mwanachama wa CCM anasifa za kuwa kiongozi- Polepole