Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Argentina, Jorge Sampaoli amekataa kutii maagizo aliyopewa na viongozi wa shirikisho la soka nchini humo, Argentina Football Association (AFA) ya kuchukua jukumu la kukinoa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20.

Uongozi wa AFA ulitoa amri, baada ya kocha huyo kurejea nchini Argentina akitokea Urusi alipokwenda kukiongoza kikosi cha timu ya taifa, ambacho kilitolewa katika hatua ya 16 bora, kwa kufungwa mabao manne kwa mawili na Ufaransa.

Amri ya kupewa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20, ilikuwa kama mtihani kwa Jorge Sampaoli, na kama angefanikiwa kufikia lengo engerejeshwa kwenye majukumu yake ya kuliongoza benchi la ufundi la timu ya taifa ya wakubwa.

Kukataa kwa kocha huyo, kutamfanya aondoke jumla katika jukumu la kuwa kocha wa timu ya taifa ya Argentina, na uongozi wa AFA utaanza mchakato wa kumsaka mbadala wake siku kadhaa zijazo.

Hata hivyo, uongozi wa AFA utalazimika kumlipa fidia Sampaoli, kwa kuvunja makubaliano ya mkataba wake, ambapo suala la kukabidhiwa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20, halikuwepo, endapo angeshindwa kufanya vyema kwenye fainali za kombe la dunia mwaka huu.

Kufuatia hali hiyo, beki wa zamani wa klabu za Deportivo La Coruña, Racing Santander na Real Mallorca Lionel Scaloni, ambaye alikua msaidizi wa Sampaoli, anatarajiwa kukabidhiwa jukumu la kuwa kocha wa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20.

Achraf Hakimi atua Borussia Dortmund
EXCLUSIVE VIDEO: Uhamiaji wataja mambo muhimu ya kuzingatia kuhusu 'PASSPORT'