Ikiwa imebaki siku moja na saa kadhaa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu zifunguliwe rasmi, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. Jakaya Kikwete ameibua mapya kuhusu mwenendo wa kampeni wa mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa.

Akiongea jana jijini Dar es Salaam baada ya mgombea wa chama hicho Dk. John Magufuli kusaini hati ya kiapo katika mahakama kuu, rais Kikwete alionesha wasiwasi wake kuwa picha zinazoonesha umati mkubwa ukimpokea Edward Lowassa katika sehemu mbalimbali zimetengenezwa.

Dk. Kikwete aliwaambia wanachama wa CCM kuwa picha halisi za umati zitaonekana Jumapili wakati chama hicho kitapozindua kampeni zake.

“Siku ya uchaguzi biashara asubuhi jioni mahesabu tu, kama watu walikuwa wanapiga picha na kuunganisha kwenye kompyuta sasa Jumapili hii mtamona picha halisi,” Alisema.

Picha ya umati uliojitokeza kwenye mkutano wa Edward Lowassa hivi karibuni

Picha ya umati uliojitokeza kwenye mkutano wa Edward Lowassa hivi karibuni

Katika hatua nyingine, Kikwete alimrushia vijembe vingine Edward Lowassa kwa kudai kuwa watanzania wote kwa ujumla wao hawawezi kununulika bali wachache tu ndio wanaoweza kununulika kwa fedha.

Kijembe hiki kinaonekana kwenda kwa Lowassa moja kwa moja kwa kuwa moja kati ya sababu ambazo chama hicho kimekuwa kikieleza kubariki uamuzi wa kulikata  jina lake wakati wa mchakato wa kura za maoni ni tuhuma za kutoa fedha kwa wanachama wa chama hicho ili wamuunge mkono.

“Mtu unaweza kuwanunua watu wachache kwa tamaa zao na wengine kwa njaa zao lakini huwezi kukinunua chama chote. Na hivyo hivyo katika kameni wataweza kuwalipa wachache lakini hawawezi kuwanunua watanzania wote. Mwisho wa siku wataamua kupigia CCM,” alisema mwenyekiti huyo wa CCM.

Hata hivyo, mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa ambaye pia alisaini hati ya kiapo Mahakama Kuu, alikataa kuongea mambo mengi mbele ya waandishi wa habari akidai watakutana jukwaani.

Simba Kujipima Kwa Mwadui FC
Everton Kusajili Beki Kisiki Kutoka River Plate